Accessibility Settings

color options

monochrome muted color dark

reading tools

isolation ruler

Ijapokuwa maelezo ya uanahabari wa upekuzi hutofautiana, kuna makubaliano mapana miongoni mwa makundi ya kitaaluma ya uanahabari kuhusu nguzo zake muhimu: hufuata mfumo maalum, huwa na kina, hutegemea utafiti asilia na uandishi wa habari ambao mara nyingi huhusisha ufichuzi wa siri. Kwa wengine, upekuzi aghalabu huhusisha matumizi mengi ya data na rekodi za taarifa za umma, huku ukiangazia haki ya kijamii na uwajibikaji.

Kanuni ya Uanahabari wa Upekuzi iliyochapishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) inaeleza hivi: “Uanahabari wa upekuzi huhusisha kuufichulia umma mambo yaliyofichwa aidha makusudi na mtu aliye na mamlaka, au yaliyofichwa bila kukusudia kwenye mlundikano wa taarifa nyingi au mazingira yanayozuia uelewa wa watu. Hutegemea matumizi ya stakabadhi na vyanzo bayana na vya siri.” Kikundi kimoja cha wanahabari wapekuzi kinachotumia lugha ya Dutch na Flemish kwa jina VVOJ kinaelezea uanahabari wa upekuzi kwa mkato: “ni uanahabari changanuzi na wenye kina.”

Baadhi ya wanahabari, kwa hakika, wanadai kuwa kwa jumla uandishi wa habari ni uanahabari wa upekuzi. Kuna ukweli fulani katika madai haya – mbinu za upekuzi hutumiwa pakubwa na wanahabari ambao huangazia nyanja maalum huku wakiripoti ndani ya muda waliopewa, na vile vile na washiriki wa “kikosi cha upekuzi” walio na wiki kadha za kushughulikia makala fulani. Lakini uanahabari wa upekuzi ni mpana kuliko hivi – ni mkusanyiko wa mbinu ambazo ni sanaa inayoweza kumchukua mtu miaka mingi kuielewa kwa ustadi. Vigezo vya juu vya utafiti na uwasilishaji wa taarifa katika tasnia ya uanahabari wa upekuzi vinathibitishwa na makala yanayonyakua tuzo za juu. Tasnia yenyewe huwa na azimio hili: udadisi wa kina unaofuatilia kwa makini sana wizi wa fedha za umma, matumizi mabaya ya mamlaka, uharibifu wa mazingira, kashfa zinazofungamana na afya, na kadhalika.

Ingawa wakati mwingine uanahabari wa upekuzi huelezewa kama tasnia, uanahabari wa kina, au unaoripoti kuhusu mradi fulani, hii isieleweke kuwa ni sawa na kile kimekuja kufahamika kwa Kimombo “leak journalism” (uanahabari wa taarifa za siri zitolewazo bila mtoaji kujitambulisha ni nani) – unahusu taarifa za mara moja anazopata mwanahabari kabla ya wanahabari wengine kupitia stakabadhi au vidokezi vilivyotolewa, kwa kawaida, na watu walio na mamlaka ya kisiasa. Yakini katika demokrasia zinazoibuka, maelezo ya uanahabari wa upekuzi yaweza yasiwe wazi, na makala mara nyingi hutajwa ni ya kipekuzi ikiwa tu yanachanganua au kuhusisha rekodi zilizotolewa pasipo mtoaji kujitambulisha. Makala yanayoangazia uhalifu au ufisadi, uchanganuzi, au hata maoni ya mtu binafsi yanaweza vilevile yakatajwa kimakosa kuwa ni uanahabari wa upekuzi.

Wakufunzi waliobobea wanashikilia kuwa uanahabari wa upekuzi ulio bora zaidi hutumia mbinu yenye umakini huku ukitegemea pakubwa vyanzo vya habari vya msingi, uundaji na ujaribishaji wa makisio, na uhakiki thabiti wa taarifa. Maelezo ya kamusi ya “uchunguzi” ni “udadisi wa kimfumo ”, ambao kwa kawaida huwezi ukafanyika kwa siku moja au mbili; udadisi wa kina huhitaji muda. Wengine huashiria kwenye mchango wa tasnia hii katika kulimbukisha mbinu mpya, kama vile matumizi yake ya kompyuta kuchanganua data na kuwasilisha taswira yake. “Uanahabari wa upekuzi ni muhimu kwa sababu hufundisha mbinu mpya, na njia mpya za kufanya mambo,” alieleza Brant Houston, mwenyekiti wa taasisi ya uanahabari ya Knight katika Chuo Kikuu cha Illinois. Brant aliwahi kuhudumu kwa miaka mingi kama mkurugenzi mkuu wa muungano wa Wanahabari na Wahariri Wapekuzi (Investigative Reporters and Editors). “Mbinu hizo hufungamana na uandishi wa habari kila siku. Kwa hiyo, unapandisha vigezo vya taaluma yote.”

Makala hii imetolewa kwenye Global Investigative Journalism: Strategies for Support, David E. Kaplan, Center for International Media Assistance, 2013. Kaplan ni mkurugenzi mkuu wa Global Investigative Journalism Network, muungano wa makundi 184 yasiyo ya faida katika mataifa 77 ambayo hufanya kazi kufadhili uanahabari wa upekuzi.

Mitazamo ya Ziada

Uanahabari wa Upekuzi ni Nini, Sura ya Kwanza kwenye Mwongozo wa Uanahabari wa Upekuzi, ambao ni mradi wa mwaka 2010 wa Global Media Programmes unaoongozwa na Konrad Adenauer Stiftung (KAS).

Makala hii imetafsiriwa na Kabugi Mbae, mwanahabari wa Kenya na mwanachama wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU).