Accessibility Settings

color options

monochrome muted color dark

reading tools

isolation ruler

Ripoti

Kutumia Utafiti wa Rununu Kuchunguzia Mgogoro wa Sudan Kusini

Ndani ya kipindi cha wiki chache, milionea wa Sudan Kusini Joseph Lugala Wani alipoteza karibu kila kitu alichokuwa nacho. Hoteli moja na maduka 10 yaliharibiwa. Yaliporwa na kuchomwa. Miezi kadha baadaye, Wani aliyegeuzwa mkimbizi wa mjini alitueleza tulipomkuta kwenye nyumba ndogo yake ya kupanga nchini Uganda, kuwa wanajeshi wa serikali ndio waliomfanyia hayo. Waliweka magurudumu ya gari ndani ya jengo na kulichoma, huku wakiteketeza hoteli ambako maafisa walikuwa wakikaa.

Timu yetu ilikuwa inaripoti kuhusu kufurushwa kwa nguvu kwa watu, uharibifu wa mali, na makazi nchini Sudan Kusini. Hii ndio nchi changa zaidi duniani, baada ya kujipatia uhuru kutoka kwa Sudan mwaka 2011. Kwa miezi kadha, tulikuwa tukisikia fununu za unyakuzi wa ardhi; baadhi ya wenzetu hata walikuwa wameshuhudia hilo wenyewe. Lakini tulitaka kujua waliohusika – na kwa kiwango gani unyakuzi huo ulikuwa umeenea.

Nikizingatia hilo, mwaka 2017 niliungana na mwenzangu Lagu Joseph Jackson, mwanahabari wa Sudan Kusini anayefanyia kazi uhamishoni, na pamoja tukaunda programu ya kutafiti kwa njia ya simu ili kuwafikia watu nchini kote. Lengo lilikuwa kuwafikia watu ambao vinginevyo hatungewapata kwa sababu ya vizuizi vya serikali, kutojua kusoma na kuandika, na umaskini. Matokeo yake yakawa mradi: Waliofurushwa.

Kuripoti Katika Maeneo Usikoweza Kufika

Sudan Kusini ilikuwa ikikandamiza vyombo vya habari. Wanahabari walitishwa, kudhibitiwa, kufungwa jela, na wakati mwingine kuuawa kwa kuripoti ukweli kuhusu mgogoro haribifu wa kijamii katika nchi hiyo. Wanahabari wengi wa nchi za kigeni – hasa waliokuwa wameandika makala zilizozikasirisha mamlaka za serikali za usalama wa taifa – walinyimwa vibali vya kazi na kukatazwa kuingia nchini, mimi nikiwemo. Kwa wanahabari waliokuwa bado ndani ya nchi, ilikuwa vigumu kwao kufika kwenye maeneo yaliyoathiriwa na mgogoro, kando na kuwa ilichukua muda mwingi na gharama kubwa. Sudan Kusini inashikilia nafasi ya 138 kati ya 180 katika fahirisi ya Wanahabari Wasio na Mipaka 2020 ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, ikiwa baina ya Palestine na Myanmar.

Wananchi wengi wa Sudan Kusini wamefurushwa na wanaishi kwenye kambi au wametafuta hifadhi nje ya mipaka ya nchi. Watu wengi hawana simu sikanu za kunakili udhalimu unaofanywa, kama zilivyotumika katika migogoro mingineo nchini Syria au Sudan. Na hata wanakilipo, wananchi wengi wanaogopa, na hawataki kujiweka katika hatari ya kukutwa na ushahidi. Lakini karibu kila mtu ana simu ya mkononi ya kawaida.

Mwahabari wa kujitegemea Carolyn Thompson akifanya utafiti na wanajeshi wa upinzani nchini Uganda mwaka 2017. Picha: Kwa hisani ya Carolyn Thompson

Hii ndiyo iliyokuwa maana kwamba kwetu sisi, na kwa wanahabari wengine wanaofanya kazi katika mazingira sawia yaliyo kandamizi, utafiti kwa njia ya simu huenda ukatoa suluhu. Mbinu ii hii huenda ikawa na umuhimu mkubwa wakati wa pandemia ya kirusi cha korona, kwani wanahabari wanapata vyanzo vilivyojiweka chini ya uangalizi au vinavyofanya kazi katika maeneo ambayo uingiaji na utokaji wake unadhibitiwa na sheria mpya. Yafuatayo ni mambo machache tuliyojifunza wakati tukifanya mradi huu ambayo huenda yakawafaa wanahabari wapekuzi wengine wanaoripoti juu ya jamii zilizo katika maeneo yasikofikika.

Utafiti Kwa Simu Katika Lugha Sita

Tulitanguliza kurekodi programu ya utafiti wetu kwa lugha sita – Kiingereza, Kiarabu, Kidinka, Kinuer, Kibari, na Kimadi. Wahojiwa wangejibu maswali kwa kubonyeza nambari kwenye simu zao, na katika visa vingine kwa kurekodi ujumbe. Utafiti huu wa simu ya mkononi ulisambazwa kupitia upigaji simu kwa kubahatisha kwenye mtandao wa kitaifa. Katika miradi mingine ya kuripoti, chaguzi tofauti huenda zikajumuisha kutuma ujumbe kijumla mtandaoni ili kuwarai watu wakubali kushiriki, au kupiga nambari za simu zilizo kwenye orodha maalum – kwa mfano kama ulikuwa na orodha ya nambari za simu za wahudumu wa afya au wafanyakazi katika sekta mahususi. Tulichagua programu ya utafiti kwa sauti iliyorekodiwa kwa sababu ya vikwazo vya watu kutojua kusoma na kuandika na changamoto za intaneti. Lakini pia unaweza ukawaruhusu watu kushiriki utafiti wa mtandaoni au kutoa majibu kupitia jumbe za sauti au ujumbe mfupi katika maeneo yaliyo na huduma bora ya simu na mtandao.

Thomas Holder na Kristen van Schie kutoka African Defence Review wakiwa kazini katika kituo cha Malakal kinachotoa ulinzi kwa raia eneo la Upper Nile, Sudan Kusini. Picha: Richard Stupart/African Defence Review

Ushirikiano Muhimu

Timu yetu ilizidi kuwa kubwa kadiri mradi wetu ulivyokua, na tuliongeza washirika kama ilivyohitajika. Tulianza kwa kupata ufadhili kutoka kwa Pulitzer Center on Crisis Reporting uliotuwezesha mimi na Jackson kuungana na Viamo, kampuni inayoendesha huduma na tafiti kupitia mitandao ya simu. Tulifanya kazi na wanatakwimu na wataalamu waliotupa ushauri wa thamani kuhusu mbinu tulizotumia.

Halafu tuliunganishwa na African Defence Review (ADR), chombo cha habari kinachoangazia usalama. ADR kilituma wanahabari nchini Sudan Kusini, na kikatusaidia kwa utafiti wa satelaiti kufuatilia uharibifu nchini kote, huku mimi na Jackson tukiripoti kutoka Uganda. Baada ya miezi mingi ya kutafiti, kuripoti, na kuunda programu ya utafiti, Al Jazeera wakaja na kuridhia kuwa wachapishaji wetu, wakihariri na kuunda picha na miundo ya midia-anuai.

Tulijifunza kupangia muda na fedha zaidi kuliko ilivyoruhusu bajeti yetu ya awali, kwa sababu ya matumizi ya mbinu mpya katika eneo lenye changamoto duniani. Tulikabiliwa na changamoto kubwa wakati tukikusanya data ya utafiti. Viwango vya kuacha kushiriki – kasi ya jinsi watu walivyoachia utafiti na kukoma kujibu – vilikuwa juu. Ni tatizo tulilotarajia, lakini sio kwa viwango tulivyoshuhudia. Wakati uo huo, uchumi wa nchi ulikuwa unaporomoka na kwa hiyo gharama ya kufanya utafiti ilikuwa inaongezeka. Tulilazimika kupunguza idadi ya maswali, kubadili mpangilio wa utangulizi, na kuomba ufadhili zaidi wa fedha ili kuhakikisha saizi ya sampuli yetu ilitosheleza ukubwa unaofaa.

Methodolojia Amini

Vile vile ilikuwa muhimu kuhakikisha kuwa makala yetu iliweka wazi kasoro za methodolojia, na sababu zetu za kuuchagua. Ulipofika wakati wa kufasili data, tulitaka kuwa na hakika kuwa uchanganuzi wetu haukuwasilisha visivyo – methodolojia yetu yenye kasoro – lakini iliyohitajika. Tulifanya kila juhudi kuunga mkono na kuthibitisha data kwa taarifa nyinginezo, yakiwemo mahojiano na watu, rekodi za umma kama vile ripoti kutoka Umoja wa Mataifa au Human Rights Watch, na kutafiti kwa kutumia picha za satelaiti. Pia tuliamua kutochukulia data kuwa muhimu kitakwimu, ikizingatiwa changamoto ya kutambua muundo wa demografia ya Sudan Kusini, na tukijua kuwa wahojiwa wetu waliegemea wanaume, vijana, na watu wanaoishi mijini ambako kuna mtandao bora wa simu. Tuliweka wazi maamuzi hayo na mapungufu kwenye methodolojia yetu, ilimradi watu wasome makala hiyo wakiwa na ufahamu huo.

Tuliwaeleza wasomaji wetu kwamba tulipiga simu kwa zaidi ya nambari 35,000 kwa kubahatisha, huku zaidi ya watu 2,900 wakisilikiza utangulizi na kuchagua lugha. Jumla ya watu 405 walikamilisha maswali yote 14 ya utafiti, ulioundwa kwa mashauriano na wataalamu wa haki za ardhi nchini Sudan Kusini na wanatakwimu. Kwa watu hao 405, asilimia 40 walisema walikuwa wamefurushwa kutoka kwenye ardhi au makazi yao tangu Disemba 2013; karibu nusu yao waliwalaumu wanajeshi wa serikali.

Tulihofia watu wangetilia shaka habari yetu, na kwa hiyo tuliwekeza wiki kadha katika kazi ya kuthibitisha ushahidi na data ya utafiti.

Uthibitisho na Ulinzi wa Chanzo cha Habari

Jambo lingine tulilojifunza ni kufanya kila juhudi ya kuthibitisha ushahidi kwa kutumia mbinu nyingi za kuripoti na kutafiti; hii ni muhimu hasa katika mradi nyeti.

Tulikusanya picha za uharibifu wa mali zilizowasilishwa na tukazihakiki kwa kutumia mbinu za upekuzi wa vyanzo vya hadharani. Tuliangalia metadata ya picha ili kuthibithisha ikiwa ilipigwa kwa kutumia simu za vyanzo vyetu. Tulilinganisha picha zilizowasilishwa na picha za satelaiti, na kupata ishara za uharibifu zilizolingana na nyakati zilizoelezewa kwenye mahojiano yetu. Tulithibitisha data kuhusu uharibifu iliyotokana na ufatifi kupitia utambuzi wa mahali kwa kutumia data, kwa kutafuta shule za msingi tulizowauliza watu wazitaje majina, na kutafuta picha za satelaiti ili kuona ikiwa kulikuwa pia na ushahidi wa uharibifu kwenye picha hizo. Katika karibu kila kisa, ushahidi ulilingana. Tulipata violezo vya uharibifu ulioenea vijijini na mijini nchini kote.

Mwanahabari Lagu Joseph Jackson akiwa kazini. Picha: Kwa hisani ya Lagu Joseph Jackson

Tulizingatia ulinzi na usalama wa vyanzo vyetu kwenye mchakato wetu. Hatukuwa na hakika ya jinsi serikali ilikuwa na uwezo wa kukatiza utafiti wetu au kusikiliza kwa siri majibu yaliyotolewa. Ili kukabili hali hiyo, tuliongeza utangulizi wenye maelezo ya kina na kumbukumbu kuwa wahojiwa walikuwa na hiari ya kukata simu wakati wowote.

Vile vile tulitafiti uwezo wa serikali wa kupeleleza, hata tukakusudia kufanyia utafiti wetu kwenye kambi za wakimbizi badala ya Sudan Kusini, ingawa hatimaye tuliamua hiyo haikuhitajika. Kulikuwa na vikwazo vya kiteknikali ambavyo Viamo ililazimika kuvitatua mwanzoni; katika baadhi ya majaribio yetu ya mwanzoni kulikuwa na ukatizaji uliotokea wenyewe ambao ulipoteza wakati na fedha pasipo kutoa majibu yoyote ambayo yangetumika. Sio wazi ikiwa ukatizaji huo ulitokana na serikali au la, lakini ulisababisha ucheleweshaji.

Matokeo ya Kuridhisha

Ulikuwa mchakato mrefu, na mara nyingi tulihisi kukata tamaa. Tulihofia kuwa data yetu ilikuwa finyu mno kiasi cha kutokuwa na maana, na tulichelewa wakati tunabadili muundo wa programu ya utafiti ili kuhakikisha watu hawakuachia katikati kufanya utafiti. Kadhalika tulihofia kuwa watu wangetilia shaka habari yetu, na kwa hiyo tuliwekeza wiki kadha katika kuthibitisha ushahidi na data ya utafiti. Vilevile tulitaka kuhakikisha kuwa makala yenyewe ilikuwa na mvuto. Tulitumia muda mwingi katika jinsi ya kusimulia na kutafuta mifano ya watu halisi ambao maisha yao yalikuwa yameathiriwa, ili kwamba makala yetu isiwe ni ya data pekee.

Juhudi zetu zilifanikiwa pakubwa – makala yetu ilifikia watu nchini kote na kuonesha takwimu za mada ambayo tulikuwa tumeisikia tu kikanda au kama hekaya. Ilisababisha kuwepo kwa mjadala katika jamii ya Sudan Kusini kuhusu haki za umiliki wa ardhi na makubaliano ya Amani, na ikashinda nafasi ya tatu katika Tuzo ya Philip Meyer ya Investigative Reporters and Editors kwa matumizi bora zaidi ya mbinu za uangalizi katika uanahabari.

Labda mbinu zetu huenda zikatumika katika nchi nyinginezo zinazokabiliwa na changamoto sawia wakati na baada ya pandemia ya kirusi cha korona; nchi ambako watu hawawezi wakasafiri salama au mamlaka zinataka kubana habari, lakini ambako pia kuna watu wengi wanaosubiria kusikiwa.

Makala hii imetafsiriwa na Kabugi Mbae, mwanahabari wa Kenya na mwanachama wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU).

Carolyn Thompson ni mwanahabari wa data wa kujitegemea anayefanya kazi akiwa Nairobi, Kenya. Yeye mara nyingi huripoti kuhusu ufurushaji wa watu, haki za binadamu, uchumi, na siasa. Kazi yake imetokea kwenye Al Jazeera, Canadian Broadcasting Corporation, France 24, na The Washington Post miongoni mwa vyombo vingine vya habari.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Republish our articles for free, online or in print, under a Creative Commons license.

Republish this article


Material from GIJN’s website is generally available for republication under a Creative Commons Attribution-NonCommercial 4.0 International license. Images usually are published under a different license, so we advise you to use alternatives or contact us regarding permission. Here are our full terms for republication. You must credit the author, link to the original story, and name GIJN as the first publisher. For any queries or to send us a courtesy republication note, write to hello@gijn.org.