Screenshot: Johns Hopkins University & Medicine Map
Kuripoti Kuhusu Kirusi cha Korona Barani Afrika: Orodha Jumuishi ya Maudhui ya Makala
Ni njia gani bora kabisa ya kufanya makala kuhusu kirusi cha korona? Chagua hoja au maudhui fulani. Haijalishi kwa kawaida huwa unaripoti kuhusu nini kwa sababu pandemia hii inajipenyeza katika karibu kila taarifa. Kutokana na hilo, taasisi ya African Centre for Media Excellence (ACME) yenye makao yake jijini Kampala, Uganda imeunda orodha ya maudhui ya taarifa kuhusu kirusi cha korona. Orodha hii inaangazia nyanja mbalimbali zikiwemo kilimo na chakula, uchumi, elimu, dini, michezo, na sanaa na burudani.
Haya hapa makundi ya maudhui hayo:
Kilimo na Chakula
- Je, ni kwa jinsi gani mshuko wa bei ya kimataifa ya bidhaa muhimu umeathiri wafanyabiashara muhimu katika nchi yako? Ni bidhaa zipi zilizoathirika zaidi? Je, athari ya mshuko wa bei imefika hadi kwenye masoko ya mashinani?
- Je, ni kwa jinsi gani baa la sasa la chakula au lile lililobashiriwa nchini mwako limezidishwa na pandemia ya kirusi cha korona?
- Je, ni nini athari ya pandemia ya kirusi cha korona kwa jamii nyonge zinazofanya kazi katika sekta ya kilimo isiyo rasmi?
- Je, ni programu zipi, iwapo zipo, ambazo zimewekwa ili kushughulikia wasiwasi wa dharura kuhusu hali ya lishe ya watoto katika familia zilizotegemea miradi ya shule ya kulisha watoto? Je, kuna michango ya misaada iliyotolewa kuziba mapengo haya ya upatikanaji wa chakula?
- Je, ni kwani jinsi gani jamii zinazotegemea uzalishaji wa chakula na ufugaji wa mifugo zinakabiliana na kuvurugwa kwa mfumo wa usambazaji wa pembejeo za kilimo na kushindwa kwao kufikia masoko ya mifugo?
- Je, jamii za wafugaji wa kuhamahama zimeathirika na kufungwa kwa mipaka? Ni kwa jinsi gani serikali yako na mamlaka za mitaa zinashirikiana na jamii hizi kuhakikisha kuwa njia za kuhamia za mifugo wao hazifungwi au kukatizwa kwa kiasi kikubwa?
- Je, mikakati ya kuhakikisha usalama wa chakula imepata hadhi zaidi kwenye orodha ya sera muhimu za nchi yako kutokana na kirusi cha korona? Ni mazungumzo gani ya sera kuhusu usalama wa chakula yanayoendelea katika serikali, asasi za kiraia, na jamii ili kuzuia kupotea kwa chakula?
- Je, ni kina nani ambao maisha na usalama wao wa chakula uko katika hatari kubwa zaidi kutokana na pandemia ya kirusi cha korona?
- Je, ni nini kimefanywa kuhakikisha mwendelezo wa usambazaji na uuzaji wa vyakula vikuu na vyenye virutubisho kamili wakati wa vipindi vya kudhibiti kirusi cha korona?
- Je, ni kwa jinsi gani kafyu, amri ya kukaa nyumbani, na usitishwaji wa usafiri wa umma umeathiri wakulima wadogo?
- Je, ni kwa jinsi gani pandemia ya kirusi cha korona imezidisha unyonge wa wakulima katika mataifa yaliyoathirika na uvamizi wa nzige hivi karibuni, unyeshaji usio wa kawaida wa mvua nje ya msimu na mafuriko? Je, ni juhudi gani zilizowekwa kuzisaidia jamii hizi kupata nafuu ikatapoisha pandemia ya kirusi cha korona?
- Je, ni bidhaa zipi zisizoharibika haraka zinazohitajika sana majijini na katika vituo vya mashinani kwa wakati huu? Je, bei imepanda ya vyakula visivyoharibika upesi kama vile mahindi, mtama, unga wa muhogo, maharagwe, njegere, njugu, na simsim (ufuta)? Je, wauzaji wanaweza kukidhi hitaji hili linaloongezeka?
- Je, ni mifumo gani ya usambazaji wa dharura wa chakula cha msaada imewekwa nchini ili kulisha jamii zilizo nyonge? Mifumo hii ni gani, ni nani anayeisimamia, na inatumika kwa lengo lililokusudiwa? Ni fursa gani zilizopo za wasambazaji chakula kushiriki juhudi hizi za kutoa msaada? Kuna changamoto zipi katika kukifikia chakula cha msaada?
- Je, ni kwa jinsi gani mbinu za kuzuia kirusi cha korona zimeathiri usambazaji wa mbegu, dawa za mifugo, mbolea, na dawa za kuua wadudu? Je, wauzaji wa kimataifa na wa nchini wa pembejeo za kilimo wanafanya nini kuhakikisha mifumo yao ya upelekaji haivurugwi kwa kiasi kikubwa?
- Je, kufungwa kwa mipaka kumekuwa na matokeo gani kwa uuzaji na ununuzi wa bidhaa za kilimo nje ya nchi kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo? Je, bei ya bidhaa za kilimo imeathiriwa na hali hii?
Uchumi na Fedha
- Je, ni kwa jinsi gani mshuko wa bei wa bidhaa zinazouzwa na kununuliwa kimataifa kama vile mafuta, gesi, madini, na chakula umeathiri uchumi wako? Ni nini kinafanywa kuweka vizuizi na kusaidia kuilinda nchi yako dhidi ya athari za mishuko hii ya bei?
- Je, nchi yako inahusika vipi kwenye mikakati ya kikanda na kikontinenti ya kukabili changamoto za kiuchumi zilizosababishwa na kirusi cha korona?
- Je, ni nani anayetoa ufadhili wa kifedha kukabiliana na athari za kirusi cha korona kwa uchumi na mapato ya serikali?
- Je, uwazi katika matumizi ya fedha unazingatiwa mabunge yanapoidhinisha bajeti za ziada na serikali kupata ufadhili mpya wa kifedha? Ni nani anayeongoza usimamizi wa fedha hizi? Je, vigezo vya uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma vinazingatiwa?
- Je, sera ya fedha ya nchi yako imebadilika ili kukabiliana na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi? Ni mabadiliko gani ya sera ya mapato ya serikali yanayofikiriwa kwa sasa?
- Je, nchi yako inafanya nini kuzuia kushuka kwa uchumi kwa kipindi cha miezi kadha au, hali ikizidi, hata miaka mingi?
- Je, biashara ndogo na zile za kiwango cha kati zinakabiliwa na changamoto zipi wakati huu wa kudhibiti kirusi cha korona?
- Je, biashara zisizotegemea mtandao kuendesha shughuli zake zinafanya mabadiliko gani kuhamishia shughuli zake mtandaoni ili kukabiliana na kufungwa kwa biashara? Je, waajiriwa wanapewa mafunzo ya kuendesha biashara mtandaoni? Ni aina gani za biashara zinazofanya hivi na kwa malengo gani? Kuhamishia biashara mtandaoni kunahitaji nini au kuna changamoto zipi?
- Je, ni nafasi gani za kibiashara nchini mwako zimeundwa na pandemia ya kirusi cha korona? Je, zimetumiwa kwa jinsi gani? Je, ni nani anayezitumia?
- Je, kufungwa kwa shughuli za utengenezaji wa bidhaa kumekuwa na athari zipi? Je, mvurugo wa usambazaji wa bidhaa umesababisha upungufu wa bidhaa zinazotengenezewa nchini au zinazoagizwa kutoka nje ya nchi? Je, mivurugo hii imekuwa na jumla ya gharama gani katika sekta ya utengenezaji bidhaa?
- Je, serikali na mamlaka za mapato zimeweka mikakati ipi kuipunguzia jamii ya kibiashara ugumu wa kulipa ushuru?
- Je, sekta za madini na mafuta zimeathirikaje na kupungua kwa kasi ya biashara? Ni nchi zipi zilizoathirika zaidi na ukosefu wa wanunuzi? Ni kwa jinsi gani mshuko wa bei za bidhaa umeathiri shughuli za madini na mafuta?
- Je, kumekuwa na ongezeko la hitaji la maji na umeme kutokana na kampeni ya kunawa mikono? Ni kwa jinsi gani kampuni zinazotoa huduma hizi zinashughulikia ongezeko hili pamoja na ombi la umma la kupunguziwa ada?
- Utekelezaji wa mkataba wa biashara huru ya kikanda barani Afrika (African Continental Free Trade Area) unatazamiwa kuanza Julai 2020. Je, majadiliano kuhusu mkataba wa kwanza wa biashara unaoshirikisha bara zima la Afrika yameathiriwa vipi na kirusi cha korona? Kuna uwezekano gani wa mkataba huu kusaidia kufufua uchumi na kuimarisha uwekezaji barani Afrika baada ya pandemia kuisha?
- Je, biashara na watu binafsi wamewekewa bima dhidi ya athari za kirusi cha korona? Kirusi cha korona ni ugonjwa mpya ambao hujaorodheshwa mahususi kwenye mikataba iliyopo ya bima, lakini je kuna nafasi ya bima kufidia kukatizwa kwa biashara, hasara ya bidhaa au kifo? Je, kampuni za bima zinaangaziaje suala hili?
Elimu
- Je, nchi yako ina mkakati upi wa kufanyisha mitihani mikuu na majaribio muhimu? Ni mbinu zipi mpya za mitihani na majaribio ya masomo zinazoangaziwa?
- Je, rasilimali za elimu bila malipo zinazotolewa na serikali, shule, na mashirika yasiyo ya serikali zinatumiwaje au kupokelewaje na familia? Kuna changamoto zipi katika kuzifikia au kutumia rasilimali hizi?
- Je, shule za umma na binafsi zinafanya au kutofanya nini ili kufadhili usomaji wa wanafunzi wakiwa nyumbani?
- Je, ni changamoto zipi zinazowakabili wazazi wenye elimu ndogo na rasilimali haba katika kufadhili usomaji wa watoto wao wakiwa nyumbani? Je, kuna usaidizi wowote kutoka kwa wizara ya elimu, shule, au mashirika ya asasi za kiraia?
- Je, wanafunzi wanakabiliana vipi na kufungwa kwa shule?
- Je, ni jamii zipi zilizo kwenye mtandao na zisizo mtandaoni ambazo zipo ili kuwasaidia walimu, wazazi na wafanyakazi wa shule? Ni habari gani zinazotolewa kwenye jamii hizi na zinatumikaje?
- Je, ni vifaa gani vilivyopo vya kuwasaidia wazazi walio na ugumu wa kusoma?
- Je, taasisi za elimu ya juu zinatumiaje mbinu za wanafunzi kusoma wakiwa mbali na vyuo? Ni changamoto zipi zilipo katika utekelezaji wa masomo ya mbali? Je, vyuo vikuu na vyuo vya kawaida vinashughulikiaje mahitaji ya wanafunzi na wakufunzi?
- Je, nini hatima ya wafanyakazi wa kawaida wa shule? Je, wangali wanalipwa mshahara? Je, wamepata usaidizi wowote kutoka kwa serikali au wasimamizi wa shule?
Utawala
- Je, mikakati ya nchi yako ya kudhibiti kirusi cha korona imehusisha makundi ambayo kihistoria yamekuwa yakitengwa na kutowakilishwa kikamilifu? Ni nani ambaye hajahusishwa? Ni nani ambaye amepuuzwa?
- Je, ni nani anayefuatilia usimamizi wa ufadhili wa kibinadamu na wa kifedha unaopewa nchi yako ili kusaidia juhudi zake za kudhibiti kirusi cha korona? Serikali yako inafanya nini kuhakikisha kuna uwazi katika matumizi ya ufadhili huu? Ni mapengo gani yaliyopo katika uwajibikaji ambayo yanaweza kuchangia utumizi mbaya wa ufadhili huo?
- Je, nini kinachofanywa kukabiliana na ukosefu wa usawa katika matumizi ya huduma za kidijitali nchini mwako ikiwa amri ya kukaa nyumbani imehamishia elimu, kazi na habari za umma mtandaoni? Je, kuna mijadala gani kuhusu uwezo wa kupata na kumudu intaneti? Je, ni vipi serikali na sekta ya kibinafsi
zinavyoshughulikia jambo hili? - Je, maagizo ya “kaa nyumbani” au “jisitiri ndani” yameathiri vipi usikilizaji na uamuzi wa kesi mahakamani? Je, amri ya watu kufungiwa kiasi au kabisa nyumbani imeathiri vipi utekelezaji wa maagizo ya mahakama?
- Je, uwezo wa watu wanyonge na maskini wa kufika mahakamani umeathiriwaje na usitishwaji wa usafiri wa umma?
- Je, nini kinachofanywa kukomesha ufisadi miongoni mwa maafisa wanaolinda sheria, wafanyakazi wa serikali, au wateule wa kisiasa walio na majukumu ya kutoa huduma kwa wakati huu? Ikiwa kuna ufisadi katika utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti kirusi cha korona, ni wa aina gani na ni nani anayehusika?
- Je, ni shughuli gani muhimu za serikali ambazo zimesitishwa au kuahirishwa kwa sababu ya pandemia ya kirusi cha korona? Hii imeathirije majukumu ya serikali, kama vile uundaji wa sheria, kufanywa kwa uchaguzi au sensa?
- Je, jamii zinazoishi kwenye maeneo yaliyo magumu kufikia yanapataje habari kuhusu kirusi cha korona? Serikali inafanya nini kuhakikisha watu wanafikia habari?
- Je, mlipuko wa kirusi cha korona umeathiri vipi uwazi wa serikali? Je, umeongeza mtiririko wa utoaji wa habari au umechangia upungufu wa uwajibikaji? Je, hili limebadilisha vipi mitazamo ya wananchi kuhusu serikali na viongozi waliochaguliwa?
- Je, mamlaka za serikali za mitaa zinapokea vipi kanuni mpya za afya ya umma za kudhibiti uenezaji wa kirusi cha korona katika majimbo yake?
- Je, afisi za serikali zisizo na mbinu za mtandao zinasimamiaje shughuli zake? Je, kumekuwa na mvurugo katika huduma na hii imeleta athari gani?
- Je, mfumo wa mahakama umekabilianaje na kirusi cha korona? Je, mabadiliko yoyote mapya yanakuwa na athari gani katika upatikanaji wa haki kwa wananchi?
- Je, kufikia sasa ni fedha kiasi gani zimetumika katika juhudi za kukabiliana na kirusi cha korona nchini mwako? Je, fedha hizo zimetumika hasa kufanya nini? Je, kiwango kile kikubwa kabisa cha fedha kimetumika wapi?
- Je, ni fedha ngapi zimepokelewa kama michango ya misaada ili kukabiliana na kirusi cha korona? Wafadhili hao ni kina nani?
- Je, hali ya watu kutotakiwa kukaribiana imeathiri vipi shughuli za serikali katika kiwango cha serikali kuu na cha serikali za mitaa?
- Je, pandemia ya kirusi cha korona imedhihirisha nini kuhuhu nguvu na mapungufu ya mifumo ya kinga ya jamii ya nchi yako?
- Je, kuna mikakati gani ya kuwalinda wafungwa dhidi ya mlipuko wa kirusi cha korona? Kama kukitokea mlipuko walikofungiwa wafungwa, ni mifumo gani ya tiba na udhibiti imewekwa? Je, kuna mipango yoyote ya kupunguza idadi ya wafungwa kwa wakati huu?
- Je, katika uundaji na utekelezaji wa mikakati ya kuzuia kirusi cha korona, serikali inahakikisha kuwa haki za wananchi zimelindwa? Je, kuna hatari zipi au uhalisia wa serikali kupitiliza au kukiuka mipaka? Hilo limepelekea vipi ukiukwaji wa haki za binadamu?
- Je, umma umechukulia vipi mikakati ya serikali ya kudhibiti uenezaji wa kirusi cha korona?
- Je, ni kwa jinsi gani serikali yako huenda inatumia juhudi za kudhibiti kirusi cha korona kukandamiza uhuru wa raia, kunyamazisha vyombo vya habari, au kujikita zaidi katika mamlaka?
Huduma ya Afya
- Je, ni kwa jinsi gani utafiti na uvumbuzi barani Afrika juu ya changamoto nyinginezo kuu za afya vinavyotumika katika kujifunzia na kutibu kirusi cha korona?
- Je, ni taratibu zipi za haki ya kiafya zimeratibishwa kwenye mifumo ya nchi yako ya kukabiliana na kirusi cha korona ili kupunguza matokeo ya afya yasiyo na usawa? Je, utofauti wa kiafya umeongezeka au kupungua kutokana na pandemia ya kirusi cha korona?
- Je, ni vielelezo gani vimechochea mikakati ya afya ya umma inayotumiwa na nchi yako kudhibiti kirusi cha korona? Je, uigaji wa vielelezo hivyo una mapungufu gani? Je, vielelezo hivyo vimebadilikaje kwa wakati kadiri vinavyotumikishwa kwa data halisi ya ulimwengu?
- Je, shughuli za kinga dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) zinaendelea wakati huu wa kudhibiti kirusi cha korona? Je, ni mikakati gani inachukuliwa kuhakikisha usalama wa watu wanaojitolea, wafanyakazi wa umma, na wateja wakati wa utoaji wa huduma za kinga?
- Je, nini kinachofanywa kuhakikisha kuwa watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi wanaweza kufikia tiba ya kutosha ya kupunguza makali ya virusi? Je, kuna changamoto zipi za kutoa tiba? Je, ni uvumbuzi upi umefanywa ili kuwajalizia dawa au kutoa dawa za miezi kadha kwa watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi?
- Je, haki za wagonjwa wanaotibiwa kirusi cha korona zinalindwa? Je, ni kwa jinsi gani huenda hofu ya kuenea kwa kirusi cha korona inachangia kukiukwa kwa haki za wagonjwa? Je, ni nani anayetetea haki za wagonjwa?
- Je, nchi yako inatekeleza mbinu zipi za usimamizi wa ukaguzi na tiba ya wagonjwa wa kirusi cha korona? Je, mifumo yake ya tiba imefanikiwa kwa kiasi gani? Je, ni changamoto zipi wanazokabiliana nazo madaktari na manesi katika kuwatibu wagonjwa wa kirusi cha korona?
- Je, ni nini kinachoendelea nyuma ya kuta za maeneo ya kitaasisi ya karantini?
- Je, nini kinafanyika mtu anapopona kirusi cha korona? Je, ni kwa muda gani watu wangali katika hatari ya kueneza kirusi? Je, sayansi inasemaje kuhusu hili, na ni nini bado hakijulikani?
- Je, ni ufadhili gani uliopo kwa watu wenye magonjwa ya afya ya akili? Je, wafanyakazi wa afya wamejiandaa vipi kwa ongezeko lililobashiriwa la ugonjwa wa akili wakati wa kudhibiti kirusi cha korona?
- Je, watu walio wanyonge kabisa na wale ambao ni vigumu kuwafikia wanapata huduma ya kupimwa na uangalizi bila malipo au kwa ada iliyo nafuu? Je, ni jamii zipi zilizo katika hatari kubwa zaidi kutokana na ugumu wa kufikia tiba?
- Je, nchi yako ina mifumo ya kuhakikisha mwendelezo wa huduma za kupanga uzazi, kuwashughulikia kiujuzi mama waja wazito, kujifungua, na baada ya kujifungua? Je, nchi yako inaweza ikahakikisha kuna tiba mwafaka ya maambukizi ya magonjwa ya zinaa?
- Je, ni kwa jinsi gani utoaji damu kwa hiari umeathiriwa na kirusi cha korona? Je, mashirika yanayoshughulika na utoaji damu yanafanya nini kuhakikisha mwendelezo usiokatizwa wa utoaji damu kwa wakati huu?
- Je, ni jukumu gani wanalofanya wahudumu wa afya wasiotambulika sana kama vile mafamasia, wasimamizi wa maabara, wahudumu wa afya ya dharura (EMTs), na wataalamu wa upumuaji wakati wa kudhibiti kirusi cha korona? Je, ni nini kimefanywa kuhakikisha usalama wao kazini?
- Je, mifumo ya afya na kiepidemiolojia nchini mwako imefadhiliwa upya na rasilimali inazohitaji kukabiliana na kirusi cha korona? Je, rasilimali hizi zimetoka wapi? Je, uhamisho wowote wa rasilimali umekuwa na athari gani kwa sekta nyinginezo?
- Je, kuvurugwa kwa biashara ya kimataifa kutaathiri usambazaji wa dawa muhimu, bidhaa dogodogo za matibabu, pamoja na vifaa? Mvurugo huo utaathiri kwa namna gani? Je, ni mifumo gani imewekwa na bodi na mamlaka za famasia kuhakikisha usambazaji thabiti wa bidhaa muhimu?
- Katika sehemu ambako mifumo ya afya imebanwa na juhudi za kudhibiti kirusi cha korona, ni majukumu gani ya uangalizi yaliyowaangukia wanawake na wasichana ambao mara nyingi hukutwa na wajibu wa kuwatunza wagonjwa katika familia zao? Je, wanawake na wasichana hawa wameathiriwaje na ongezeko la mzigo huu? Ni ufadhili gani uliopo kwa ajili yao?
- Mapema mwezi Machi, serikali nyingi zilitangaza vizuizi vya usafirishaji wa bidhaa na viungo vya matibabu nje ya nchi zao. Hii ina maana kuwa upelekaji wa paracetamol, baadhi ya viuavijasumu, na dawa za kawaida kutoka kwa wauzaji wakubwa zaidi wa bidhaa hizi hadi Afrika umekatizwa. Je, nchi yako tayari imeanza kudhurika kwa sababu hii? Je, ni mipango gani mbadala imewekwa kuziba pengo lililosababishwa na upungufu wa bidhaa zitokazo nje ya Afrika?
- Je, kirusi cha korona kimebadili au kuupa sura ujumbe wa sekta ya umma kuhusu elimu ya afya na lishe? Wananchi kote nchini wanapokeaje ujumbe huu mpya?
- Je, kufungwa kwa taasisi za elimu ya juu kumekuwa na athari kwa ufadhili ambao wanafunzi wa udaktari na unesi hutoa kuzisaidia hospitali? Wanafunzi wengi hutoa msaada unaohitajika sana kwa kufanya majukumu kama vile kuwaangalia wagonjwa, kuwapa vitanda, na vilevile dawa. Je, hili limeongeza shinikizo na mahitaji kwa wafanyakazi wa hospitali? Je, wakufunzi wa taasisi zilizofungwa wanajitoa kuwasaidia wafanyakazi hawa? Ikiwa ndio, kwa njia gani?
- Je, ni mikakati gani imewekwa kupunguza hatari ya uambukizaji wa wafanyakazi wa afya hospitalini kote nchini? Je, wafanyakazi wa afya wamejiandaa vipi kwa ajili ya kirusi cha korona?
- Je, vituo vya mawasiliano ya simu kuhusu kirusi cha korona vinaendeleaje?
- Je, mfumo wa kitaasisi wa karantini hasa unafanyaje kazi? Je, ni nini huendelea katika maeneo kunakoshukiwa kuwa na visa vya kirusi cha korona? Je, watu wanaorudi kutoka mataifa yenye hatari kubwa ya maambukizi wanawekwa kwenye karantini?
- Kumekuwa na ripoti za utoaji rushwa kwenye viwanja vya ndege na maeneo mengine ya kuingia nchini na watu ambao hawakutaka jamaa zao au wao wenyewe kuwekwa kwenye karantini. Je, hili lilifanyikaje? Je, ni maafisa gani wa serikali wenye ushawishi au wananchi binafsi waliohusika?
- Je, hospitali za rufaa za kitaifa na za kikanda zina uwezo kiasi gani katika kuzingatia idadi ya vitanda vya wagonjwa mahututi, ujuzi na vifaa? Je, hospitali za rufaa za kikanda na hospitali za kibinafsi zinajiandaa vipi kwa uwezekano wa mlipuko mkubwa wa kirusi cha korona? Je, ni mipango gani mbadala imewekwa kufadhili huduma za ukaguzi na tiba ya wagonjwa?
- Je, ni mipango gani mbadala imewekwa ikiwa itatokea kwamba hospitali zimefurika wagonjwa wa kirusi cha korona? Je, wafanyakazi wa afya na wataalamu wanasema nini kuhusu mipango hii?
- Huku rasilimali zikielekezwa katika kuzuia na udhibiti wa kirusi cha korona, mataifa yamejiandaa vipi kwa milipuko ya sasa na ya siku zijazo ya magonjwa? Je, kirusi cha korona kimezidisha mzigo wa magonjwa uliopo kwa sasa?
- Je, kirusi cha korona kimedhihirisha nini kuhusu nguvu na mapungufu ya mfumo wa afya nchini?
- Je, ni wapi duniani kunakofanywa juhudi za kutafuta tiba au kinga dhidi ya kirusi cha korona?
- Je, upimaji wa kirusi cha korona unafanyikaje?
Leba
- Je, ni wafanyikazi gani wenye ujuzi wameshuhudia upungufu wa hitaji la huduma zao tangu kutokea kwa pandemia ya kirusi cha korona?
- Je, kuna matarajio gani kwa wafanyakazi wasio wa kudumu na wale wazururao wakitafuta kazi, katika kipindi cha kudhibiti kirusi cha korona? Je, serikali inashughulikiaje ukosefu wa ulinzi wa kijamii na kiuchumi kwa watu hawa?
- Je, ni majukumu gani ya jumla kuhusu afya na usalama waliyo nayo waajiri katika nchi yako? Je, ni nini kinachofanywa kuhakikisha waajiri wanazingatia maagizo ya serikali ya kuwalinda waajiriwa wao?
- Huku huduma za leba zifanywazo na raia wa nchi za nje zikiwa zimesimamishwa, ni ufadhili gani uliopo kwa watu walioajiriwa kupitia kampuni zitoazo huduma hizi? Ni msaada gani, ikiwa upo, walio nao kutoka kwa vituo vya kidiplomasia vya nchi yako?
- Je, ni sekta zipi zilizoathiriwa zaidi na kuvurugwa kwa usafiri na shughuli za kazi? Je, ni sekta za elimu, utalii, burudani, hoteli, kieletroniki, na bidhaa za starehe? Je, hii imekuwa na athari gani kwa waajiriwa wafanyao kazi kwenye sekta hizi? Je, hii itakuwa na athari gani kwa mipango ya uwekezaji na upanuaji wa biashara?
Maisha ya Watu
- Je, pandemia ya kirusi cha korona imeathiri upelekaji wa ufadhili wa kibinadamu kwa nchi yako? Je, rasilimali zilizokusudiwa kwa ufadhili zinaelekezwa kusaidia juhudi za kudhibiti kirusi cha korona? Hii inaleta matokeo gani?
- Je, kirusi cha korona kimedhihirisha nini kuhusu ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi katika nchi yako? Je, wadau wa serikali na wasio wa serikali wanashughulikia vipi uhalisia uliojitokeza?
- Je, uangalizi na ufadhili wa manusura wa dhuluma ya kijinsia vimevurugwa na pandemia ya kirusi cha korona? Je, hii inaibua hatari zipi kwa watu walio na uwezekano mkubwa wa kuathirika, hususan wanawake na wasichana?
- Je, mikakati ya kuzuia kirusi cha korona inatekelezwaje katika jamii zinazoishi kwenye mazingira yenye uhaba wa maji? Je, kuna mashirika yoyote ya serikali na yasiyo ya serikali yanayoshughulika kutoa maji safi na salama kwa wakati huu?
- Je, kirusi cha korona kimeathiri jinsia za watu kwa namna gani? Je, wanawake wameathiriwaje na kipindi cha kudhibiti kirusi cha korona, kufungwa kwa shule, na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi?
- Je, watu wenye ulemavu wameshughulikiwa kikamilifu katika kipindi hiki cha kudhibiti kirusi cha korona? Je, wanaweza kufikia habari kupitia vyombo vya habari, jamii na vyombo vya serikali vinavyowafaa? Je, ni mikakati gani ya ufadhili kwa ajili ya watu wenye ulemavu iliyopo kutoka kwa serikali, asasi za kiraia, na mashirika ya kijamii?
- Kuna hofu kuwa vituo vya wakimbizi huenda vikapata pigo la kirusi cha korona kutokana na ukosefu wa huduma muhimu kama vile matibabu na vyanzo vya maji salama ya kunywa. Je, mataifa wenyeji wao yamejiandaa vipi kwa uwezekano huu?
- Je, mikakati ya kudhibiti kirusi cha korona inatekelezwaje katika kambi na vituo vyenye idadi kubwa ya wakimbikizi?
- Je, kufungwa kwa mipaka kumeathiri vipi maisha ya kijamii na kiuchumi ya jamii zinazoishi mpakani?
- Je, serikali yako inashughulikia vipi mahitaji ya watu wanaoishi kwenye makazi yasiyo rasmi? Je, ingali inatoa huduma nyinginezo ili kuzuia, kugundua, na kutibu magonjwa katika jamii hizi?
Watu
- Je, ni “mashujaa gani wa kimya” kwenye vita ya nchi yako dhidi ya kirusi cha korona? Je, ni nani aliye kwenye mstari wa mbele katika mawasiliano ya umma, mikakati ya udhibiti ya sekta ya afya, au juhudi za jamii za kukabiliana na kirusi cha korona? Orodhesha wengi kadiri unavyoweza.
- Je, huwa vipi muuguzi anapokuwa kwenye mstari wa mbele akitibu wagonjwa wa kirusi cha korona?
- Je, ni uvumbuzi gani wa kijamii umefanywa au unafanywa ili kusaidia watu wanyonge zaidi katika jamii wakati huu wa pandemia?
- Je, watu waliokutwa na kirusi cha korona wanapokeaje tiba na kuwepo kwao hospitalini?
- Je, kirusi cha korona ni nini kupitia kwa macho ya wagonjwa hawa au jamaa zao na wale wanaowatunza?
- Je, kirusi cha korona ni nini kupitia kwa macho ya washukiwa ambao hawakukutwa na kirusi cha korona?
- Je, kirusi cha korona ni nini kupitia kwa macho ya wagonjwa ambao wameshapona?
- Je, viongozi wa nchi yako wameweka mikakati gani kujihakikishia usalama wao binafsi?
Kazi za Umma na Miundo Mbinu
- Je, ni miradi gani mikubwa ya miundo mbinu imeathiriwa na kufungwa kwa shughuli za kazi na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi? Je, ni tarehe gani za malengo muhimu ambazo hazitaafikiwa? Je, ni mikakati ipi iliyopo kuhakikisha rasilimali za fedha na watu zipo ili kukamilisha miradi hii kwa wakati?
- Je, miradi mikubwa ya miundo mbinu inayofadhiliwa na taasisi za kifedha za Uchina, au kutekelezwa na kampuni za Uchina, itaathiriwaje na kirusi cha korona?
Dini
- Je, jamii za kidini nchini mwako zinakabilianaje na pandemia ya kirusi cha korona?
- Je, mikakati ya udhibiti wa kirusi cha korona yamebadilisha huduma za kidini na utoaji wa misaada kwa wenye mahitaji?
- Je, watu wamezuiwa kufika kwenye maeneo matakatifu, maabadi yanayohusishwa na mtu au tukio takatifu, na maeneo mengine ya ibada za kitamaduni za kiafrika? Je, wafuasi wa ibada za kitamaduni wanapokeaje mikakati hii?
- Je, kirusi cha korona kimepunguza au kuongeza nafasi iliyopo baina ya sayansi na dini katika nchi yako? Je, ni mijadala gani inayoendelea kuhusu huu “mgongano wa kimawazo”?
- Je, viongozi wa kidini nchini mwako wanapewa ufadhili gani kufanya huduma za sakramenti na matambiko kwa jamii na watu wanaohitaji msaada? Je, amri ya kukaa nyumbani na mikakati ya udhibiti wa kirusi cha korona inawaruhusu kuendelea na huduma hii? Kama sivyo, wanafanya nini kukidhi mahitaji ya watu?
- Je, ni huduma gani za uchungaji ambazo viongozi wa kidini wanaweza wakatoa kwa wakati huu, na wanafanyaje hivi?
- Je, kuna viongozi wowote wa kidini wanaofanya kazi muhimu – iwe chanya au hasi – katika kudhibiti uenezaji wa kirusi cha korona? Hii imekuwa na athari gani?
- Je, mashirika ya kidini yanafanya jukumu gani wakati wa baa hili?
- Je, ibada ina mwonekano gani katika nchi yako wakati huu?
Michezo, Sanaa na Burudani
- Je, kuna programu za msaada nchini mwako za kufadhili wachezaji wenye mahitaji kutokana na kusitishwa kwa shughuli za michezo?
- Je, kirusi cha korona kimebadili shughuli za mwili za watu na mazoea yao ya kufanya mazoezi ya mwili?
- Je, ni mapato kiasi gani yamepotea kutokana na kufutwa kwa matamasha ya muziki, hafla za sanaa, na shughuli za michezo? Je, ni mikakati gani imewekwa ili kujipatia mapato haya siku za usoni?
- Je, wanamichezo wanafanya nini katika kipindi cha udhibiti wa kirusi cha korona? Je, vilabu na mameneja wanafanya nini kupunguza uwezekano wa kuumia kwa wachezaji, hasa katika michezo ambayo wachezaji hugusana?
- Je, ni kwa jinsi gani watu wahusikao kwenye sanaa ya maonyesho wanavyokabiliana na kusitishwa kwa shughuli zao? Je, ni nani aliyeathirika zaidi?
- Je, watu mashuhuri kwenye michezo na burudani wanatumiaje majukwaa yao kuelimisha na kuhabarisha umma kuhusu mbinu za kujikinga dhidi ya kirusi cha korona? Je, ni nani anayeongoza harakati hii na kumekuwa na matokeo gani?
- Je, ni wasanii gani wanaotumia vifaa vya mtandaoni ili kusalia wakiwa wameunganika na hadhira yao wakati huu? Je, kuna yeyote anayetumia vyombo hivi kujipatia mapato?
Mkusanyiko
- Je, ni kwa jinsi gani mataifa ya bara Afrika yamekabiliana na pandemia ya kirusi cha korona?
Makala hii ilitokea mara ya kwanza kwenye tovuti ya ACME, na imechapishwa hapa kwa idhini. Tuma hoja zaidi na mapendekezo kwa tovuti ya ACME, kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii au kwa baruapepe.
Makala hii imetafsiriwa na Kabugi Mbae, mwanahabari wa Kenya na mwanachama wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU).
African Centre for Media Excellence ni shirika huru la kitaaluma lisilo la faida na lenye makao yake Kampala. Nia yake ni kuleta ubora katika uandishi wa habari na mawasiliano kwa umma barani Afrika. ACME hutumia mbinu ya muda mrefu ambapo semina za mafunzo ya vitendo huambatanishwa na ushauri na ukurufunzi.