Accessibility Settings

color options

monochrome muted color dark

reading tools

isolation ruler

Ripoti

Vidokezi vya Kuchunguzia Kirusi Cha Korona Afrika

Wanahabari wapekuzi wa Afrika wanafanya kazi muhimu ya kutoa maelezo na ufafanuzi wa pandemia ya kirusi cha korona inayokua barani, na kuziwajibisha serikali.

Makala za upekuzi zimezindua baadhi ya serikali zilizokuwa zimezubaa katika utayari wake kwa ajili ya kirusi cha korona. Kadhalika, makala za upekuzi za hivi karibuni zimezindua utumizi mbaya wa fedha kupitia tiba bandia na wanakandarasi wenye hila.

Lakini viashiria vya hivi karibuni vya ongezeko la maambukizi, makadirio ya kutokea kwa vifo zaidi ya Shirika la Afya Duniani (WHO), na kukithiri kwa ukosefu wa ajira vimezua wasiwasi kuhusu athari za kirusi cha korona katika mataifa 55 ya bara Afrika. Mnamo Mei, WHO pia lilionya kuhusu kitanzi kinachoweza kuangamiza ambapo kirusi cha korona kingeathiri usalama wa chakula, huku ukosefu wa chakula kwa upande wake ukidhoofisha mifumo ya kinga ya watu, na hivyo kufanya kirusi kuwa hatari zaidi. Pia kuna wasiwasi zaidi kuhusu ukosefu wa rasilimali za afya na kuenea kwa umaskini kote barani.

Huku utendakazi wa jamii ya uanahabari wa upekuzi ukikumbwa na changamoto, wanajopo wanne walielezea mikakati ya kufanya makala kuhusu pandemia ya kirusi cha korona wakati wa mkutano wa GIJN wa mtandaoni kwa jina Tishio kwa Afrika, uliofanyika wiki iliyopita na kuhudhuriwa na wanahabari 260 kutoka mataifa 57.

Ujumbe wa msingi wa jopo ulikuwa wazi: Anza na nyanja za habari unazozifahamu, fanya upekuzi wako kuwa rahisi, shirikiana na wenzako, wategemee wanasayansi, na uwaangazie watu, hata katika uandishi wa habari wenye uzito wa sayansi na data.

Dayo Aiyetan, mkurugenzi mkuu wa  International Centre for Investigative Reporting (ICIR) nchini Nigeria, alisema wanahabari kwenye nchi yake walikuwa na athari za moja kwa moja katika uhamasishaji wa mikakati ya serikali, baada ya kukanusha madai ya awali kutoka kwa baraza la mawaziri kuwa “Nigeria ilikuwa tayari kukabiliana na pandemia ya kirusi cha korona.”

“Hali iliimarika kwa sababu ya wanahabari kuangazia kilichokuwa kinaendelea,” alisema. “Kuhusiana na mawasiliano ya serikali, kulikuwa na ishara tangu awali kutoka kwa wanahabari kuwa hali haingeendelea kama kawaida.”

Katika wiki ya kwanza ya Aprili, ICIR ililinganisha kiwango kidogo cha marupurupu ya hatari ya kila mwezi (US$13.64) walichopata madaktari wa Nigeria waliotibu wagonjwa wa kirusi cha korona, na jumla ya $460 na $825 walizolipwa madaktari nchini Sierra Leone na Liberia, mtawalia, wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola mwaka 2015. Kadhalika, ICIR walitanzua mfumo mgumu wa utoaji bima ya kirusi cha korona kwa madaktari wa Ghana ili kutafuta ulinganisho wa sasa wa $361 katika viwango sawa vya ada ya marupurupu ya hatari. Makala hiyo ilisababisha ongezeko mara tano la marupurupu ya hatari kwa baadhi ya madaktari wa Nigeria wiki mbili tu baadaye. Hii inaonesha aina ya mbinu rahisi na makini ambayo Aiyetan alisema ilifanikiwa katika siku za awali za pandemia.

Mtazamo uliokubalika na wote kwenye mkutano wa mtandaoni – ambao ulikuwa mjadala wa nane kwa lugha ya Kiingereza katika mfululizo wa makala ya GIJN kwa jina Kuchunguza Pandemia ya Kirusi cha Korona  – ni kuwa wanahabari wa Afrika wamefanya vema katika kuchanganua mikakati ya serikali dhidi ya kirusi cha korona, na hasa katika kukanusha taarifa za uongo. Lakini wengi wa wanahabari wanataabika kutambua na kupata habari zinazohusu uwajibikaji, zaidi ya zile za ajenda ya habari za kila siku.

Dk Peter Mwesige, mkurugenzi mkuu wa African Centre for Media Excellence, alisema kuwa uwazi na kutambua bayana shaka kwenye taarifa ilikuwa muhimu katika kuripoti kuhusu kirusi cha korona, kwenye muktadha wa imani ya umma na usahihi.

“Hii ni taarifa ambayo bado inaendelea; hakuna uhakika kuhusu takwimu, na hata wataalamu wenyewe hawakubaliani,” alisema. “Kwa hiyo lazima tuitambue shaka katika kazi yetu, pamoja na ukweli ambao hatujui.”

Mnamo Aprili, Mwesige na timu yake walichapisha orodha ya mkusanyiko wa mawazo unaojumuisha maudhui mbalimbali ya makala zinazoweza kufanywa na wanahabari barani Afrika, tokea athari juu ya mifumo ya usambazaji kwenye kilimo hadi kwa wajibu walio nao viongozi wa kidini. Mwesige alisema orodha hiyo ilitolewa, kwa sehemu, ili wanahabari waweze kupanua habari zao kwenye nyanja za habari zilizopo wakati wanaripoti kuhusu athari pana za kirusi cha korona, na kwa sehemu, kuwasaidia wanahabari kuyafahamu matokeo mengi ambayo pandemia ya kirusi cha korona huenda ikasababisha, zaidi ya yale yahusuyo afya.

“Kama vyombo vya habari, tunahitaji ufahamu zaidi wa usanifu wa namna kirusi cha korona kinavyokabiliwa katika mataifa tofauti barani Afrika,” alisema. “Na tunahitaji kuuliza maswali yale yale tena na tena. Na tunahitaji kufuata pesa zinakokwenda – je, zilitumiwa hasa kwa kusudi lililowekwa?”

Joshua Olufemi, mwasisi wa Dataphyte nchini Nigeria alisema ijapokuwa wanahabari wa Afrika wana majukwaa mengi ya chanzo na uchanganuzi wa data, wanapaswa kuwaangazia watu, hata wanapokuwa wakipitia takwimu nyingi kwenye nakala za Excel.

Ikizingatiwa kutakuwa na ucheleweshaji wa stakabadhi muhimu za kidijitali kama vile za ukaguzi wa mahesabu za kipindi cha kirusi cha korona, Joshua alisema wanahabari wanaweza ziba pengo hili kwa kushirikisha juhudi za watu wengi kwenye mitandao ya kijamii na kutegemea data iliyo nje ya mtandao kutoka kwa vyanzo vilivyo kwenye nyanja za kawaida za habari.

Wakati huo huo,  Mia Malan, mwasisi na mhariri mkuu wa Bhekisisa Centre for Health Journalism nchini Afrika Kusini, aliezea mikakati kadha mahususi juu ya makala za afya, ikiwemo vidokezi vya “kuihadaa” hadhira ili isome au kutazama matini ya sayansi ya matibabu ambayo vinginevyo ingeiepuka.

Malan alisema makala za simulizi na sayansi zilikuwa na nafasi bora zaidi ya kuishirikisha hadhira – na Bhekikisa pia ilikuwa ikizidi kutumia miundo ya makala ya video kuwavutia watu ambao hawangesoma makala hiyo kamwe.

Bhekikisa ni shirika huru la habari linalojulikana kwa ufumaji wake wa ushahidi uliohakikiwa, pamoja na uandishi wa simulizi. Tayari, limetoa makala yenye athari kuhusu tiba ya kirusi cha korona ambayo haijathibitishwa kama vile mlundikano wa vipimo vya “tiba ya Madagascar, na mahojiano na wanasayansi walio kwenye mstari wa mbele katika juhudi za Afrika Kusini za kukabiliana na kirusi cha korona. Vile vile wamechapisha makala ya kusikitisha kuhusu meya wa jiji kuu moja aliyenuia kutumia fedha za umma kununua “chanjo” ambayo haikuwapo.

Mojawapo ya makala za awali kuhusu namna hospitali zilivyokabiliana na pandemia ya kirusi cha korona barani Afrika ilifanywa Asha Mwilu, aliyekuwa mhariri wa miradi maalum katika Citizen TV nchini Kenya. Mwilu alisema alilazimika kujiweka karantini kwa siku 14 baada ya kuripoti kutoka kwenye wadi za wagonjwa wa kirusi cha korona jijini Nairobi.

Vidokezi vya haraka kutoka kwa jopo:

 • Anza na nyanja na vyanzo vya kawaida vya habari wakati mkijadili chunguzi zinazohusiana na pandemia ya kirusi cha korona – kila sehemu ya maisha itaathiriwa. Kuna uwezekano nyanja kama vile kilimo, dini na elimu zisiangaziwe kikamilifu, au ziwe kiingilio adimu kwenye makala muhimu zinazohusu uwajibikaji.
 • Zifuate fedha na ufuate sayansi kwenye utafiti wako, lakini uwaangazie watu unapoandika taarifa yako. Kadiri utakavyoweza, wakilisha wahusika wote kupitia wanadamu, wakiwemo wanasayansi, waathiriwa, na maafisa wa serikali.
 • Kuwa mwazi kwa hadhira yako kuhusu shaka iliyo kwenye data, mambo usiyoyajua, na kweli ambazo huenda zikawa zimepitwa na wakati muda ambao makala yako inaonekana.
 • Kujiepusha na hatari hakumaanishi utupilie mbali simulizi ya makala yenye mnato. Makala za simulizi zenye kina zinaweza zikafanywa kwa simu au kupitia mtandao wa Skype. Mwanahabari mmoja wa Bhekisisa alitumia zaidi ya saa tano kwenye simu akizungumza na chanzo muhimu cha habari ili kuonyesha jinsi ulivyofanya kazi mfumo wa kufuatilia na kuwatambua watu ambao huenda walitangamana na wale walioambukizwa.
 • Jizoeshe kutafuta ushauri wa wanasayansi juu ya maswali kuhusu dhana za kisayansi. Kwa taarifa za msingi zinazoweza kutegemewa, tumia tovuti za kuaminika kama vile Mayo Clinic. Kwa utafiti, tumia rasilimali kama vile PubMed.
 • Linganisha udhibiti wa kirusi cha korona wa serikali yako na jinsi ilivyodhibiti epidemia za hapo kabla.
 • Angaza macho kwa mikoa, majimbo, na majiji ambayo huenda yanabana makusudi viwango vya kirusi cha korona kwa sababu za ndani za kisiasa. Tambua kuwa baadhi ya wanahabari tayari wanakabiliwa na unyanyasaji na kuzuiliwa kwa kuchunguza mwenendo huu.
 • Tafuta matatizo yaliyosababishwa na mtiririko wa athari za kirusi cha korona miezi sita baadaye, na uangalie ikiwa idara za serikali zinafanya vivyo hivyo katika mipango yake.
 • Pale ambapo utoaji wa data rasmi huenda ukacheleweshwa au kubanwa, fikiria juu ya kukusanya data mpya ukiwashirikisha watu wengi kupitia mtandao wa kijamii, au kwa kutumia stakabadhi zisizo mtandaoni.
 • Tafuta kufanya mahojiano na wagonjwa walioruhusiwa kuondoka hospitalini na ambao hawakukutwa na kirusi cha korona. Kuna uwezekano mkubwa utawapata rahisi na watazungumza kwa uwazi kuhusu uzoefu wao pindi warudipo nyumbani.
 • Shirikiana na mashirika ya habari wenza, hasa kwenye makala zilizo na vipengee vinavyozidi ujuzi wako, au vinavyovuka mipaka ya taifa lako.

Makala hii imetafsiriwa na Kabugi Mbae, mwanahabari wa Kenya na mwanachama wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU).

Rowan Philp ni mwanahabari wa GIJN. Rowan alikuwa mwanahabari mkuu wa zamani wa Sunday Times nchini Afrika Kusini. Kama mwanahabari wa mambo ya nchi za kigeni, ameripoti kuhusu habari, siasa, ufisadi, na migogoro kutoka kwa nchi zaidi ya 24 duniani.

Republish our articles for free, online or in print, under a Creative Commons license.

Republish this article


Material from GIJN’s website is generally available for republication under a Creative Commons Attribution-NonCommercial 4.0 International license. Images usually are published under a different license, so we advise you to use alternatives or contact us regarding permission. Here are our full terms for republication. You must credit the author, link to the original story, and name GIJN as the first publisher. For any queries or to send us a courtesy republication note, write to hello@gijn.org.