Accessibility Settings

color options

monochrome muted color dark

reading tools

isolation ruler

GIJN Africa: Usalama na Ulinzi Barani Afrika

Katika asili yake yenyewe, uanahabari wa upekuzi ni tasnia yenye hatari ambayo huwaweka wanahabari na wahariri kwenye hatari mtandaoni na nje ya mtandao.

Wanahabari wanaochimbua maasi ya maafisa wa serikali fisadi na maajenti wa ulinzi wakandamizaji hukabiliwa na vitisho vinavyolenga kuwakomesha au kudhibiti vyombo vya habari vyao hali kadhalika.

Ili kuwalinda wanahabari dhidi ya hatari za usalama na ulinzi, baadhi ya mashirika ya Afrika na ya kimataifa yameunda programu zinazotoa msaada kwa wapekuzi walio matatani, ama katika mataifa ya Afrika maalum ama barani kote.

Africa Human Rights Network

Africa Human Rights Network huendesha programu ya uhamishaji hadi kwenye majiji salama ya Dar es Salaam na Benin. Huduma hii hutolewa kwa wanahabari wapekuzi na watetezi wa haki za binadamu walio hatarini barani Afrika, ili kuwawezesha kuendelea na kazi yao katika kipindi cha uhamisho. Huduma hizi zinajumuisha usafiri, makazi na riziki, msaada wa matibabu na bima, ufadhili wa kisaikolojia, ujenzi wa uwezo na mafunzo, mwendeleo wa kazi kwa muda uhamishoni, programu za ubadilishanaji na uanzishwaji wa mitandao, na marejeo salama na mwendeleo wa kazi katika nchi yake mwenyewe.

African Freedom of Exchange Network

African Freedom of Exchange Network (AFEX) ni mtandao wa mashirika ya uhuru wa kujieleza 15 katika kanda ya kusini mwa jangwa la Sahara yanayofanya kazi kwa karibu ili kukuza na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari katika eneo hilo. Mashirika hayo pia ni wanachama wa International Freedom of Expression Exchange (IFEX). Mtandao huu hukuza uhuru wa kujieleza na haki za binadamu barani Afrika kupitia utetezi na kampeni, na ujenzi wa uwezo ili kuhakikisha ufanisi wa wanachama wake na makundi ya uhuru wa kujieleza mengineo katika eneo hilo.

Article 19

Likiwa na makao yake Uingereza, Article 19 hufanya kazi duniani kote katika kukuza haki za uhuru wa kujieleza na uhuru wa habari. Shughuli zake hujumuisha utengenezwaji wa vigezo vya sheria, changanuzi za kisheria, na ukosoaji wa sheria za kitaifa na mashtaka katika mahakama za kimataifa na za nyumbani kwa niaba ya watu na makundi ambayo haki zao zimedhulumiwa. Katika kusini mwa jangwa la Sahara, lina afisi za kikanda nchini Senegal na Kenya na huendesha programu za kieneo mbili katika magharibi mwa Afrika na kanda ya Afrika mashariki.

Association for Media Development in South Sudan

Sudan Kusini ni mojawapo ya maeneo hatari zaidi ya kufanya kazi ya uanahabari kusini mwa jangwa la Sahara kwani serikali yake ya kijeshi huelekea kukandamiza uanahabari wowote unaoikosoa kwa kuwashutumu wanahabari kuwa si wapenda amani au wanawafadhili waasi. Katika mazingira magumu haya, Association for Media Development in South ni mojawapo ya mashirika mengi yanayotetea uhuru wa vyombo vya habari nchini humo, likifanya kazi kwa karibu na mashirika mengine nchini Sudan Kusini na washirika wa kimataifa.

Committee to Protect Journalists — Africa (CPJ Africa)

Committee to Protect Journalists (CPJ) ni shirika la kimataifa lisilo la faida ambalo jukumu lake ni kulinda haki za wanahabari za kuripoti habari wakiwa salama na bila hofu ya kulipizwa kisasi. Kazi ya CPJ Africa inajumuisha kunakili masuala ya usalama, kutoa ushauri wa kiusalama na vifaa kwa wanahabari walio hatarini, na utoaji wa huduma za mwitikio wa dharura.

Free Press Unlimited

Free Press Unlimited ina programu mbili zinazolenga kutoa ufadhili wa dharura kwa wataalamu wa habari, wanahabari, na mashirika ya habari ulimwenguni kote. Hazina ya Reporters Respond emergency fund hutoa msaada wa moja kwa moja kwa wanahabari na mashirika ya habari, unaowawezesha kurejelea kazi zao haraka iwezekanavyo wakabiliwapo na janga. Hazina ya Legal Defense Fund huwafadhili wataalamu wa habari walio katika matatizo ya kisheria, kwa mfano wakati wanahabari au familia zao zinapokabiliwa na mashtaka au kifungo jelani na hawawezi kumudu kupata wakili au gharama ya kesi.

Human Rights Network for Journalists – Uganda

Human Rights Network for Journalists – Uganda ni shirika lisilo la faida lililoanzishwa mwaka 2005. Hujumuisha wanahabari wabobezi na walio hai wanaofanya kazi ili kusaidia wanahabari wanaokabiliwa na ukiukwaji wa haki zao za kikatiba na uhuru wa kimsingi. Shirika hili huendesha utafiti, na kufuatilia na kunakili vitisho na mashambulizi dhidi ya wanahabari, na vilevile matumizi mabaya ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Uganda. Kadhalika hutoa msaada wa kisheria kwa wanahabari ambao kazi zao zimewatia katika hali ambayo wanahitaji msaada wa kisheria.

International Media Support (IMS)

IMS hulinda haki za wanahabari na hushughulika ili kuhakikisha wanaweza kufanya kazi kwa usalama katika nchi ambako wanahabari wanadhulumiwa na kushambuliwa kwa kufanya kazi yao au pale ambapo migogoro huzidisha hatari ya ufuatiliaji wa taarifa. Kupitia hazina ya Safety Fund, IMS hutoa ufadhili wa papo hapo kwa wanahabari wanaohasiriwa kutokana na matokeo ya moja kwa moja ya kazi yao.

Media Defence

Media Legal Defence Initiative (hivi karibuni itakuwa Media Defence) huendesha hazina ya dharura inayowasadia wanahabari, wanablogu, na vyombo vya habari huru kulipia ada za kisheria, na hutoa utaalamu wa kisheria wa mawakili wanaotetea kesi. Wanahabari, wanablogu na mawakili wanaweza kutuma maombi ya ufadhili hapa. Shirika hili lenye makao yake London vilevile linaunda mtandao wa mawakili katika mashariki, magharibi na kusini mwa Afrika kama sehemu ya Digital Rights Advocates Project. Mawakili hushughulikia kesi za uhuru wa kujieleza mtandaoni zinazowalenga wanahabari, wanablogu na mashirika ya habari. Kwenye tovuti yake, Media Defence pia ina msururu wa nyenzo za rasilimali kuhusu haki za kidijitali na uhuru wa kujieleza kote barani Afrika.

South African National Editors Forum (SANEF)

Wanachama wa shirika hili la Afrika Kusini lisilo la faida ni wahariri, wanahabari waandamizi, wakuu wa vyombo vya habari, na wakufunzi wa uanahabari waandamizi. Lengo kuu la SANEF ni kuwa mwakilishi na sauti ya kuaminika ya uanahabari nchini Afrika Kusini, na vilevile kulinda na kukuza uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari nchini humo ambao ilikuwa vigumu kuupata. SANEF ni mtoa maoni wa mara kwa mara kuhusu masuala ya uhuru wa vyombo wa habari anayeheshimika nchini Afrika Kusini. Semi zake mara nyingi huchukuliwa kama usemi wa mwisho wa tasnia ya uanahabari. Hufanya kampeni dhidi ya sheria zinazotishia kuminya nafasi ya vyombo vya habari, huendesha miradi ya mafunzo, hutetea masuala ya vyombo vya habari vya jamii, na kushirikiana na mashirika mengine ya maendeleo ya vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza. Uanachama wake ni kupitia uteuzi na huhitaji malipo ya ada ya kila mwaka. Hutunza orodha ya utafiti kuhusu nafasi ya vyombo vya habari na stakabadhi za sera nchini Afrika Kusini.

Tanzania Human Rights Defenders Coalition

Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC) ulianzishwa mwaka 2010 ili kuimarisha usalama na ulinzi wa watetezi wa haki za binadamu katika taifa hili la Afrika Mashariki. THRDC hujitahidi kuongeza usalama, heshima, na utambulikanaji wa watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania kupitia ulinzi, ujenzi wa uwezo, na utetezi.

The Totem Project

Totem ni jukwaa la kujifunzia la mtandaoni lililoundwa kupitia ushirikiano baina ya Greenhost na Free Press Unlimited. Hutoa kozi za elimu kuhusu usalama wa kidijitali na faragha, na vifaa vinavyohusiana na mbinu kwa wanahabari, wanaharakati, na watetezi wa haki za binadamu katika mazingira salama ya darasa la mtandaoni. Jukwaa la Totem limeundwa kwa kutumia programu ya Open edX MOOC (Massive Open Online Course). Jukwa lenyewe limeundwa liwe salama na kuhifadhi faragha kwa kukusanya kwa kipimo kidogo data kuhusu watumiaji wake na pia kwa kutumia mbinu ya usimbaji fiche ya kisasa iliyo salama ili kuzuia usikilizaji kwa siri wa mawasiliano.

Voluntary Media Council of Zimbabwe (VMCZ)

VMCZ ni muungano wa wanahabari, wachapishaji, vyumba vya habari, na makundi ya asasi za kiraia yanayofanya kazi kwenye nafasi ya vyombo vya habari nchini Zimbabwe. Ulianzishwa mwaka 2007 na hufanya kazi kama shirika linalojidhibiti lenyewe kwa vyombo vya habari nchini humo. Hupatanisha na kushughulikia malalamiko dhidi ya mashirika ya habari na huhudumu kama kiunganishi baina ya vyombo vya habari, serikali, na wahusika wengine wa kisiasa. Hutoa mafunzo tendeshi kwa wanahabari ili kufadhili ukufunzi wa kitaalamu usioegemea upande wowote na ujenzi wa ujuzi; miradi mingi ya mafunzo yake imeangazia uanahabari wa upekuzi. VMCZ pia huandaa Media and Investigative Journalism Awards, ambazo ndizo tuzo za vyombo vya habari kuu zaidi nchini Zimbabwe.

Makala hii imetafsiriwa na Kabugi Mbae, mwanahabari wa Kenya na mwanachama wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU).

Kwa mengi kuhusu usalama na ulinzi, tembelea GIJN Help Desk.