GIJN Africa: Ufadhili wa Kifedha
Uanahabari wa upekuzi siku zote umekuwa wenye gharama kubwa. Huku tasnia hii ikizidi kukumbwa na hali ngumu ya kiuchumi, mashirika mengi ya habari ya faida yamekoma kutengea upekuzi wa habari fedha nyingi kama ilivyokuwa hapo kabla.
Mashirika mengi yasiyo ya faida yameingilia kati ili kujaza pengo hilo. Ijapokuwa mengi ya mashirika hayo ni ya nyumbani, mengine ni ya kimataifa lakini yaliyo na operesheni zinazojikita barani Afrika ambazo zinalenga kutoa msaada wa kifedha ili kufadhili uanahabari wa upekuzi katika eneo zima.
African Centre for Media Excellence (ACME)
Makao ya ACME ni Kampala, Uganda, na lina programu zinazotoa ufadhili wa kifedha kwa uanahabari wa upekuzi, na pia hutoa mafunzo kwa wanahabari barani Afrika ili wabobee katika kazi ya upekuzi. Lengo kuu la ACME ni kufanya vyombo vya habari viwe jukwaa lenye ufanisi zaidi kwa utoaji wa habari kuhusu masuala ya umma, kifaa cha kufuatilia mamlaka rasmi, na uwanja wa mijadala ya umma yenye kina. Katika programu zake za ufadhili wa kifedha, ACME mara nyingi hushirikiana na mashirika ya kimataifa yasiyo ya faida kama vile Ford Foundation, Revenue Watch Institute, Population Reference Bureau na MacArthur Foundation.
African Media Initiative (AMI)
African Media Initiative lilizinduliwa mwaka 2008 ili kuimarisha vyombo vya habari kote barani Afrika ili vichukue jukumu kubwa zaidi katika utawala wa kidemokrasia na maendeleo ya kiuchumi. Hufanya hivi kupitia mipango inayokuza uhuru, ushirikiano, wingi, na uendelevu wa kifedha. Shughuli zake kuu zinajumuisha kufanya kazi na wamiliki wa vyombo vya habari vya Afrika na wasimamizi ili kuimarisha uwezo wao wa kukabiliana na mielekeo na changamoto za uanahabari, huku ikitoa nafasi za mafunzo kwa wanahabari, ufadhili wa kifedha kwa uandishi wa habari, kutetea mabadiliko katika sera ya vyombo vya habari, kufanya utafiti kuhusu vyombo vya habari, na kujihusisha na uundaji wa matini kwa ushirikiano. AMI pia huandaa African Media Leaders’ Forum, ambao ni mkutano wa kila mwaka wa wamiliki wa vyombo vya habari, wanahabari, na wadau wengine ili kujadili masuala muhimu.
DW Akademie
DW Akademie ndilo tawi la kimataifa la maendeleo ya vyombo vya habari la Deutsche Welle, shirika la habari la kimataifa la umma la Ujerumani. Barani Afrika, hufadhili vyombo vya habari vya kale, vituo vya radio vya kijamii, na wanablogu katika mataifa 18. Shughuli za DW Akademie huangazia kuimarisha vyombo vya habari vinavyojitegemea na vilivyo na vigezo vya juu, na maendeleo endelevu ya mifumo ya mafunzo kwa wataalamu wa vyombo vya habari. Hutoa ufadhili wa kifedha ili kuendeleza uhuru wa kujieleza na kupata habari, hasa kwa teknolojia za kidijitali.
Fojo Media Institute
Fojo Media Institute ni shirika linalojitegemea lenye makao yake katika Linnaeus University nchini Sweden lakini lina uwepo wake kimataifa. Hufanya kazi na washirika wa kitaifa na kikanda ili kuimarisha uanahabari huru, unaojitegemea na wenye utaalamu. Fojo hufadhili vyumba vya habari na mashirika mengine ya habari, na pia wanahabari binafsi, ili waweze kujitegemea kifedha na kisiasa. Husaidia katika kuunda mbinu endelevu za biashara na hutoa huduma nyinginezo nyingi za ufadhili kwa vyombo vya habari. Kwa sasa linafanya kazi katika mataifa matano – Kenya, Ethiopia, Somalia, Rwanda, na Zimbabwe – lakini limefanya na kufadhili miradi katika mataifa mengine mengi.
Ford Foundation
Ford Foundation ni shirikia kubwa la Marekani lisilo la faida lililo na afisi za kikanda katika Nairobi, Lagos, na Johannesburg. Hufadhili uanahabari wa upekuzi unaowajibisha viongozi na taasisi, uandishi wa habari unaozipa sauti sehemu za jamii zilizotengwa au kunyamazishwa, na miradi ya ubunifu inayolenga kuunganisha na kuwafikia watu wengi kadiri inavyowezekana. Ford hupokea mapendekezo yasiyoagizwa. Makataa yao ya ufadhili wa kifedha yanaendelea. Kiwango cha ufadhili wa kifedha huwa ni kati ya $50,000 na $1.25 milioni.
Hivos
Hivos ni shirika la maendeleo la kiholanzi lililo na uwepo wake kimataifa. Hutoa ufadhili wa kifedha kwa mashirika ya habari ambayo kazi zake zinaambatana na malengo na mambo ambayo Hivo huangazia, zikiwemo haki za wanawake na nishati iwezayo kutumika tena na tena. Hivos hasa linavutiwa na mashirika bunifu ya habari, uanahabari unaoangazia suluhisho mbadala kwa matatizo ng’ang’anivu. Huendesha vituo vikuu viwili: Nchini Kenya, katika kanda ya Afrika Mashariki, na nchini Zimbabwe, katika kanda ya Afrika Kusini. Vile vile lina afisi za kitaifa nchini Afrika Kusini, Zambia, Uganda, na Malawi.
International Women’s Media Foundation(IWMF)
Ufadhili wa kifedha wa shirika hili lililo na makao yake Washington, DC, Marekani huwalenga wanahabari na wapigapicha wa kike. Hujumuisha mafunzo kuhusu usalama, nafasi za uandishi, msaada wa dharura, ufadhili wa kimasomo, na ufadhili wa kifedha. Miongoni mwa miradi ya ufadhili wa kifedha ya IWMF ni Fund for Women Journalists na Emergency Fund. Fund for Women Journalists hufadhili nafasi za elimu, uanahabari wa upekuzi, na miradi ya maendeleo ya vyombo vya habari. Emergency Fund hutoa msaada kwa wanawake walio hatarini kutokana na kazi yao ya uanahabari. Aina zote mbili za ufadhili hupokea maombi kwa mwendeleo.
Irish Aid
Irish Aid ni mpango rasmi wa msaada wa maendeleo wa kimataifa wa serikali ya Ireland ambao hutoa ufadhili kwa miradi ya maendeleo katika “mataifa washirika wakuu”, huku mshirika mmoja tu (Vietnam) akiwa nje ya Afrika. Hutoa ufadhili wa kifedha kwa mashirika ya habari yasiyo ya serikali kama sehemu ya juhudi zake za kukuza utawala bora, haki za binadamu, na uwajibikaji. Barani Afrika, mataifa washirika wakuu wake ni Ethiopia, Malawi, Kenya, Mozambique, Sierra Leone, Uganda, Tanzania, na Zambia. Pia lina uwepo wake katika Liberia, Afrika Kusini, na Zimbabwe.
Luminate
Luminate ni shirika la msaada lililoanzishwa mwaka 2018 na ambalo lilitokana na Omidyar Network. Hutoa ufadhili wa kifedha usio wa faida na uwekezaji wa faida kwa mashirika na huduma za kiteknolojia na kidijitali za kiraia zinazowawezesha watu kushiriki katika utawala, kupokea huduma wanazohitaji, na kuwaajibisha walio mamlakani. Kuhusiana na vyombo vya habari na uanahabari, hulenga kufadhili mashirika ya habari yasiyo ya faida na ushirikiano baina ya wanahabari, wanasayansi wa data, na mawakili; miundo mipya ya uanachama; juhudi za ubunifu za kukabiliana na habari za uongo zinazotolewa makusudi; na njia mpya za kufadhili uhuru wa vyombo vya habari. Makao makuu yake ni London na lina afisi Nairobi, Kenya. Kwa sasa linaangazia mashirika yanayofanya kazi katika mataifa matatu ya kusini mwa jangwa la Sahara: Kenya, Nigeria, na Afrika Kusini. Hata hivyo, liko radhi kufadhili miradi yenye mnato nje ya mataifa lengwa. Kiwango cha ufadhili huwa tofauti.
Media Development Investment Fund (MDIF)
MDIF ni hazina ya uwekezaji isiyo ya faida inayolenga vyombo vya habari vinavyojitegemea katika mataifa ambako upatikanaji wa vyombo vya habari huru na vinavyojitegemea unatishiwa. Shirika hili hutoa mikopo ya riba na mauzo ya asilimia fulani ya biashara kwa wawekezaji ili kupata mtaji. Hili hushirikishwa na usaidizi wa kiteknikali kwa kampuni za habari zinazotoa taarifa, habari, na mjadala ambao watu wanahitaji ili kujenga jamii huru na zinazostawi. Lengo lao ni kuzisaidia kifedha kampuni ili ziwekeze katika mustakabali wao na kukuza biashara stahimilivu na zenye ushindani.
Media Foundation for West Africa (MFWA)
MFWA ni shirika la maendeleo ya vyombo vya habari lisilo la serikali linalofanya kazi katika mataifa yote 16 ya Afrika Magharibi. Lina programu ya uhuru wa kujieleza, na vilevile mradi wa vyombo vya habari na utawala bora unaotoa mara kwa mara nafasi za mafunzo na kufadhili uanahabari wa upekuzi kupitia misaada ya kifedha. Mnamo mwaka 2018, lilizindua West Africa Network for Investigative Journalists, na huandaa hafla ya kila mwaka ya West Africa Media Excellence Conference and Awards.
Media Institute of Southern Africa (MISA)
MISA lilianzishwa mwaka 1992 na ni muungano wa matawi ya kitaifa 11 katika Jamii ya Maendeleo ya Kanda ya Afrika Kusini. Makao yake yako Windhoek, Namibia. Shughuli za MISA hulenga kukuza vyombo vya habari huru, vinavyojitegemea, na vinavyojitanua kwenye eneo zima kupitia utetezi, ujenzi wa uwezo kwa wafanyakazi wa vyombo vya habari, ufuatiliaji wa uhuru wa vyombo vya habari, kampeni kuhusu uhuru wa kujieleza na haki ya kupata habari, na kutoa msaada wa kisheria. Shughuli hutofautiana katika kila tawi la kitaifa, huku utekelezaji wa programu ukitegemea hali ya kisiasa na mahitaji katika kila taifa. Tovuti yake ina kituo cha rasilimali kinachojumlisha changanuzi, sheria na ripoti. Matawi ya MISA katika Botswana, Malawi, Zambia, na Zimbabwe pia yana tuzo za kitaifa za vyombo vya habari zinazokuza ufanisi katika maudhui ya masuala mbalimbali.
Money Trail Grants
Nafasi za ufadhili za Money Trail zinazotolewa na Journalismfund.eu na washirika zinayalenga makundi ya ushirikiano ya wanahabari wa Afrika, Asia, na Uropa ili wachunguze mtiririko wa kifedha haramu baina ya mipaka ya kijiografia, matumizi mabaya ya ushuru, na ufisadi katika Afrika, Asia, na Uropa. Journalismfund.eu pia hukubali ushirikiano wa baina ya mipaka ya kijiografia barani Afrika na Asia kwa makundi ya wanahabari kutoka mataifa angalau mawili. Kuna nafasi tatu za kutuma maombi mwakani 2020, huku makataa yakiwa ni Machi 16, Juni 15, na Septemba 14.
Open Society Foundations
Open Society Foundations ni mojawapo wa wafadhili wa kibinafsi wakubwa zaidi wa miradi ya vyombo vya habari duniani kote. Afisi yao ya Afrika iliyoko London hufanya kazi kwa karibu na oparesheni nne zake za kanda ya Afrika na afisi za kitaifa. Oparesheni za kikanda hufadhili mashirika ya habari, miungano, harakati, na wanahabari ambao miradi yao inaendana na maeneo lengwa yao. Hakuna mfumo wa kutuma maombi mahali pamoja lakini programu za kikanda mara kwa mara huchapisha mialiko ya kutuma maombi. Programu hizo zinajumuisha Open Society Initiative in East Africa, Open Society Initiative in West Africa, Open Society Initiative in Southern Africa, na Open Society Foundation for South Africa.
Pulitzer Center
Ufadhili wa Pulitzer Center wa Persephone Miel fellowships uko wazi kwa wanahabari walio nje ya Marekani wanaotaka kuripotia vyombo vya habari vya Kiingereza vya Marekani wakiwa nchini mwao. Ufadhili huo hutoa msaada wa kifedha kwa miradi ya uanahabari “inayoangazia masuala yenye athari za kijumla kwenye nchi asili ya anayetuma maombi na inayotoa mtazamo mpana, kuliko ripoti fupi binafsi zinazoangazia matukio ambayo huenda yakawa na athari kuu au za papo hapo kutoka katika eneo la matukio.” Kadhalika, ufadhili wake wa Rainforest Journalism Fund hutoa msaada wa kuripoti kuhusu misitu inakonyesha mvua wakati wote kwa mwaka mzima katika Amerika ya Kilatini, Afrika, na Asia. Katika mwaka 2019, hazina hii ilianza kuwazia maombi kutoka kwa wanahabari wa Afrika wanaoripotia mashirika ya nyumbani na ya kikanda.
Swiss Agency for Development and Cooperation
Kama sehemu ya ushirikiano wa maendeleo na eneo la global South (maeneo ya Amerika ya Kilatini, Asia, Afrika, na Oceania), shirika la maendeleo la kimataifa la Uswizi huendesha zaidi ya miradi na mipango 800 katika maeneo ya afya na mafunzo, kazi na uvumbuaji wa mapato, maendeleo ya vijijini, mageuzi ya serikali, na mageuzi ya utawala. Hufanya kazi kukuza utawala wa sheria, haki za binadamu, na haki, katika kufadhili juhudi endelevu za maendeleo na kupunguza umaskini. Huendesha programu inayofadhili uanahabari wa upekuzi nchini Tanzania.
Taco Kuiper Grants
Ufadhili huu hutolewa ili kuchochea uanahabari wa upekuzi katika magazeti ya Afrika Kusini. Husimamiwa na idara ya uanahabari katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand, huku jumla ya ZAR 350,000 (takriban $23,000) zikitolewa kila mwaka kwa wanahabari wapekuzi nchini Afrika Kusini. Wafadhili hufikiria kuhusu kiwango chochote ambacho kimesadikishwa kwenye ombi la kutaka ufadhili. Hata hivyo, wao hupokea tu miradi ya uandishi yenye kina na upana – ikiwemo miradi ya uandishi wa vitabu – inayoangazia masuala ya kisasa yanayoathiri Afrika Kusini.
Wits Africa-China Reporting Project
Mradi huu unaongozwa na idara ya uanahabari ya Chuo Kikuu cha Witwatersrand, Johannesburg, Afrika Kusini. Hulenga kuimarisha ubora wa kuripoti kuhusu masuala baina ya Afrika na Uchina kwa kutoa nafasi za kujenga uwezo kwa wanahabari. Mradi wenyewe hutoa ufadhili, msaada wa kifedha kwa warsha za mafunzo na nafasi nyinginezo kwa wanahahabari wa Afrika na Uchina ili wachunguze mienendo changamani na kufichua masuala ambayo hayajaangaziwa hapo kabla. Ufadhili huo ambao hutolewa nyakati zote mwakani huwa ni kati ya $300 na $3,000.
Makala hii imetafsiriwa na Kabugi Mbae, mwanahabari wa Kenya na mwanachama wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU).