Accessibility Settings

color options

monochrome muted color dark

reading tools

isolation ruler

Dayo Aiyetan, Mkurugenzi Mkuu wa International Centre for Investigative Reporting (ICIR). Picha: Kwa hisani ya ICIR

Ripoti

Jinsi ICIR Nchini Nigeria Linavyoshinikiza Uwajibikaji Katika Kukabili Kirusi cha Korona

Shirika moja la uanahabari wa upekuzi lisilo la faida nchini Nigeria, International Centre for Investigative Reporting (ICIR), limepitiliza katika mbinu zake za kuchunguza jinsi Nigeria inavyokabiliana na kirusi cha korona.

Kwenye mahojiano na mhariri wa GIJN Africa Benon Herbert Oluka, mkurugenzi mkuu wa ICIR Dayo Aiyetan anaeleza kazi wanayofanya. Aiyetan, ambaye ni mwanahabari mpekuzi, mshauri katika vyumba vya habari, na mkufunzi wa vyombo vya habari atakuwa anazungumza kwenye mkutano wa mtandaoni wa GIJN, Investigating the Pandemic: The Threat to Africa, utakaofanyika Alhamisi, Mei 14, saa tatu asubuhi majira ya EDT.

Umekuwa ukichunguza habari kuhusu kirusi cha korona kwa wiki takriban sita sasa. Ni uchunguzi upi ambao umekuwa na athari kubwa zaidi?

Uchunguzi wa kwanza ni makala yetu ya data kuhusu ugavi wa fedha, ambayo ilichunguza juhudi za utoaji wa msaada wa kifedha kwa familia zenye mahitaji. Rais alikuwa ameagiza kuwa naira 20,000 ($51) zipewe familia maskini kulingana na Sajili ya Kitaifa ya Jamii inayoorodhesha watu maskini zaidi nchini Nigeria. Lakini uchunguzi wetu ulibaini kuwa watu waliokuwa wakipokea msaada kutoka kwa serikali walikuwa chini ya nusu ya idadi ya wale walioorodheshwa kwenye sajili.

Takwimu za data pia zilionyesha ukosefu wa usawa katika ugavi wa fedha. Familia nyingi zinazoishi kwenye majimbo ya kaskazini mwa Nigeria zilikuwa zikipata msaada kuliko familia zinazoishi kusini mwa Nigeria. Hii iliilazimu serikali kutafuta namna yenye usawa ya kutoa msaada wa chakula kwa wananchi wengi kadiri ilivyowezekana.

Taswira: ICIR

Vile vile kuna makala yetu kuhusu marupurupu ya hatari wanayopata madaktari na wafanyakazi wengine wa afya. Katika maeneo mengine, madaktari walipata marupurupu ya chini sana hata kufikia naira 5,000 ($13.64) kila mwezi. Tulilinganisha kiasi hiki na kile madaktari katika mataifa mengine ya Afrika Magharibi walichopata – $361 nchini Ghana, $460 nchini Sierra Leone na $825 nchini Liberia. Kufuatia makala yetu, serikali kuu na za majimbo zilirekebisha hali hiyo ndani ya wiki chache.

Kwangu binafsi, makala ambayo huenda ina athari kubwa zaidi ni ile iliyomkosoa waziri wa afya ambaye alitia chumvi utayari wa Nigeria katika kukabiliana na mlipuko wa kirusi cha korona. Alitembelea hospitali moja mjini Lagos na kutangaza kuwa Nigeria ilikuwa tayari. Shirika la Afya Duniani (WHO) pia likaimba wimbo uo huo. Hata hivyo, uchunguzi wetu ulionyesha kuwa Nigeria haikuwa hata na vituo mwafaka vya kuhifadhi wagonjwa ambao wangetengwa, na haikuwa tayari kukabili baa la kiafya ambalo lingesababishwa na kirusi cha korona. Naamini ukosoaji wetu wa waziri wa afya ulichangia katika mbinu mpya ya serikali. Kumekuwa na uwazi zaidi katika utoaji wa taarifa za kuaminika kwa wananchi na sasa, jopokazi la Rais kuhusu Kirusi cha Korona huiarifu nchi kila siku.

Habari ya kirusi cha korona ilianza kama habari ya afya kabla ya kuwashirikisha wanahabari wengine wote wakati kikienea duniani kote. Kama kitengo cha upekuzi ambacho kimetoa makala mbalimbali, mliwezaje kuangazia masuala yanayofungamana na kirusi cha korona ambayo hatimaye yalikuwa na athari?

Shirika la ICIR linaendesha chumba kidogo cha habari. Hatuna wanahabari majimboni isipokuwa tu katika jiji kuu la Abuja. Fauka ya hayo kulikuwa na amri ya kukaa nyumbani. Kwa kuwa kila mwanahabari alitoa taarifa kutoka eneo tofauti, tuliweza kupata mtazamo mpana wa kilichokuwa kinaendelea katika eneo lote la jiji kuu la Nigeria.

Lakini hatukuwa tunaangazia habari kote nchini kwani ni mambo mengi yaliyokuwa yanaendelea. Kwa hiyo, tuliwaendea wanahabari wa vyumba vingine vya habari tuliowahi kufanya kazi nao kwenye miradi ya upekuzi iliyofadhiliwa, na tukakubaliana wawe wakitupa taarifa kuhusu masuala maalum. Baadaye tulichapisha kwa pamoja. Tulifanya hivi hususan katika siku za awali wakati tukiangazia namna serikali ilivyokabiliana na pandemia ya kirusi cha korona. Tulifichua matukio mengi ya usimamizi mbaya wa awali wa harakati za kupambana na kirusi cha korona, kukanwa, na kufichwa kwa taarifa kuhusu visa vya kirusi cha korona.

Hebu tueleze kuhusu baadhi ya makala ya upekuzi ambayo mmefanya wakati wa amri ya kukaa nyumbani na jinsi mlivyoyafanya…

Makala kuhusu kurundikana kwa wafungwa gerezani na hatari ya kutokea kwa mlipuko wa pandemia magerezani, yajulikanayo kama vituo vya kurekebishia tabia nchini Nigeria, yalifanywa kwa njia ya siri angalau katika jela moja. Siwezi nikatoa maelezo zaidi ila kusema tu kwamba mwanahabari wetu aliingia kwenye jela kuu la Maiduguri na akaweza kupata taswira ya kile kingetokea ikiwa wafungwa hawangepewa vifaa vya kujikinga na idadi yao kupunguzwa.

Makala nyingine ya upekuzi tulifanya ilikuwa kuhusu harakati za serikali ya jimbo la Akwa Ibom za kukabiliana na pandemia ya korona. Tulifahamu kilichokuwa kinaendelea na tukampata mwanahabari tuliyemwamini ili awe akitutaarifu. Uchunguzi huu ulikuwa muhimu kwa sababu serikali daima ilikuwa ikikana uhalisia wa mambo huku ikizuia upimaji kufanyika na kuwataabisha wafanyakazi wa afya. Uchunguzi wetu ulifichua haya yote.

Jambo la kuvutia ni kwamba afisa mmoja wa serikali aliyekuwa amefuatilia taarifa zetu kuhusu pandemia ya kirusi cha korona aliwasiliana nasi kutoka jimbo la Akwa Ibom ili kutupa habari za kilichokuwa kikiendelea. Kwa kuwa hatukuwa na mwanahabari wetu huko, tulitafuta mwanahabari tuliyemwamini na kumwelekeza kwa afisa huyo.

Changamoto mojawapo ya wanahabari wanaoripoti kuhuhu kirusi cha korona imekuwa usahihi wa takwimu. Je, kuna wakati wewe au timu yako mmekumbana na changamoto hii? Mliikabili vipi?

Mfano unaokuja upesi akilini ni makala tuliyofanya kuhusu sajili ya kijamii ya watu maskini. Serikali ilikuwa imekataa kutoa takwimu kamili kuhusi idadi ya familia. Watu wengi, wakiwemo wanahabari, walikuwa wakinukuu takwimu tofauti ambazo hazingethibitishwa. Sisi tulibahatika. Tuliendelea kutafuta na hatimaye tukapata chanzo katika mahali palipofaa aliyetupa data iliyokuwa kwenye stakabadhi ya serikali. Baada ya kuthibitisha kuwa stakabadhi hiyo ilikuwa halali, tulitumia takwimu hizo na serikali haingeweza kukana.

Ni changamoto gani kubwa zaidi mmekabiliana nazo mkifanya uchunguzi wakati wa pandemia ya kirusi cha korona?

Naamini ni pingamizi tulizokumbana nazo tukiripoti kwenye mstari wa mbele, hasa katika hospitali na vituo vya kutibia wagonjwa waliotengwa. Tulitaka kueleza habari za wafanyakazi wetu wa afya na jinsi walivyomudu kutibu wagonjwa wa kirusi cha korona, marupurupu ya maslahi waliyopewa, iwapo walikuwa na vifaa binafsi vya kujikingia, na vifaa vya matibabu vya kufanyia kazi. Twaweza tukaelewa kuwa serikali haingetaka baadhi ya mapungufu katika tiba kwa wagonjwa wa kirusi cha korona kuwekwa wazi lakini hizi ni habari zinazohitaji kuelezwa.

Changamoto nyingine inahusiana na habari za ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa amri ya kukaa nyumbani. Kwa kuwa wanahabari wengi hawana magari, wakati mwingine uwezo wetu wa kufanya makala tunayotaka hubanwa. Hata hivyo, tulijifunza upesi na kukabiliana nayo.

Je, kuna vifaa na rasilimali ambazo zimekusaidia wewe na timu yako katika juhudi zenu za kufanya upekuzi wakati wa pandemia?

Wakati mwingine, vifaa hivyo huenda vikawa programu kama vile Twitter, au [zana tumizi ya simu] kama Truecaller na Wayback Machine. Kwa baadhi ya makala yaliyohusu uthibitishaji wa taarifa – na zimekuwa nyingi – tumetumia TinEye na huduma ya Google ya kuthibitisha uhalisia wa picha. Katika siku za awali za pandemia na baada ya kuwekwa amri ya kukaa nyumbani na viwanja vya ndege kufungwa, tulitumia Flightradar24 kufuatilia safari za ndege. Kwa mfano, tulipokuwa tukichunguza alikokuwa Abba Kyari, mkuu wa zamani wa wafanyakazi wa rais wa Nigeria, aliyefariki kutokana na kirusi cha korona, tulitumia Flightradar24 kupata tarehe ya siku aliyosafiri na ni wapi alikokwenda. [Tanbihi ya mhariri: Alifariki baadaye mwezi huo.]

Ni fursa gani kwa wanahabari wapekuzi walizokosa kutumia ambazo ungetaka wazizingatie kuanzia sasa na kuendelea?

Watumie data sio tu kuiwajibisha serikali bali pia kuweka ajenda, na kushawishi uundaji wa sera za serikali. Kwa mfano, serikali ililegeza amri ya kukaa nyumbani nchini Nigeria wakati maambukizi yalikuwa yanaongezeka. Wanahabari wanapaswa kukiweka kitendo hicho cha serikali katika muktadha kupitia kile ambacho data inaonyesha. Kwa sasa katika ICIR, tunafuatilia data kuhusu maambukizi na kufanya makala tukionyesha ikiwa kulegezwa kwa amri ya kukaa nyumbani kunastahili au la.

Taswira: ICIR

Kadhalika, sidhani wanahabari nchini Nigeria wanatumia data vya kutosha katika kuweka ajenda kwenye sekta za afya, elimu, miundo mbinu na kadhalika. Makala mojawapo tunataka kufanya hapa ICIR inahusu data ya elimu, hususan idadi ya shule na wanafunzi walioko shuleni. Tunataka kuilazimisha serikali ianze kufikiria kuhusu mustakabali wakati shule zitafunguliwa. Tunataka kutumia data hii kukadiria ni shule ngapi zaidi serikali inapaswa kujenga, maanake watoto wetu wanahitaji kudumisha umbali unaotakikana baina ya kila mmoja wao na mwenzake watakapokuwa shuleni. Wanahabari wanaweza wakatumia data kwa jinsi hii kuweka ajenda, na kushawishi uundaji sera katika karibu kila sekta ya uchumi.

Wakati wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo Vya Habari ulisema kuwa wanahabari na mashirika ya habari yanapaswa kuvumbua mbinu mpya za kufanya kazi ili yaweze kuambatana na mazingira yaliyopo na hivyo kuweza kuendelea baada ya pandemia kudhibitiwa. Ni mbinu kama zipi ulizozungumzia?

Wanahabari lazima wajifunze mbinu mpya na nafuu za kutoa taarifa hasa wakitumia teknolojia. Kwa wakati huu, kazi ya uanahabari wa upekuzi – na aina yoyote ile ya uanahabari – inaendeshwa na teknolojia. Kwa hiyo, wanahabari lazima wakumbatie zana za teknolojia na wasitegemee mbinu nzee na za kale. Hivyo basi badala ya kuhangaika na kutembea huku na kule tukitafuta vyanzo vya habari, data au stakabadhi, yapasa tujifunze kuwa mengi ya haya twaweza tukayapata mtandaoni.

Makala hii imetafsiriwa na Kabugi Mbae, mwanahabari wa Kenya na mwanachama wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU).

Benon Herbert Oluka ni mhariri wa GIJN Africa na mwanahabari wa Uganda aliyebobea katika nyanja tofauti za uanahabari. Yeye ni mwasisi mwenza wa The Watchdog, kituo cha uanahabari wa upekuzi katika nchi yake, na mwanachama wa African Investigative Publishing Collective.

 

Republish our articles for free, online or in print, under a Creative Commons license.

Republish this article


Material from GIJN’s website is generally available for republication under a Creative Commons Attribution-NonCommercial 4.0 International license. Images usually are published under a different license, so we advise you to use alternatives or contact us regarding permission. Here are our full terms for republication. You must credit the author, link to the original story, and name GIJN as the first publisher. For any queries or to send us a courtesy republication note, write to hello@gijn.org.