Accessibility Settings

color options

monochrome muted color dark

reading tools

isolation ruler

Rasilimali

» Mwongozo

COVID-19: Ushauri wa Kitaalamu Kuhusu Mitazamo ya Kuchunguzia

Kufuatia mikakati isiyo ya kawaida inayochukuliwa ili kukabili mlipuko wa kirusi cha korona, kazi ya wanahabari wapekuzi ya kuchunguza matumizi mabaya ya mamlaka na unyanyasaji wa wanyonge imekuwa muhimu zaidi wakati huu. Katika janga hili linaloenea kwa kasi, wanahabari wapekuzi wanapaswa kuanzia wapi? Ni vifaa na mbinu gani zilizo muhimu katika kuchunguzia kirusi cha korona?

GIJN ilizungumza na wanahabati wabobezi katika jamii yetu ya ulimwengu – wakiwemo wataalamu wa kuchunguza habari za uongo zitolewazo makusudi, mifumo ya usambazaji, na vifaa vya vyanzo vya hadharani – na kuwauliza watoe ushauri wao kwa wanahabari wenza kuhusu kile wanapaswa kuwa wanachunguza wakati huu wa mlipuko wa kirusi cha korona. Hivi ndivyo walivyotuambia:

Miranda Patrucic

Naibu Mhariri Mkuu, Regional Stories and Central Asia, Organized Crime and Corruption Reporting Project 

Patrucic ni mtaalamu kuhusu ulanguzi wa fedha na makundi ya kihalifu. Hufanya kazi kutoka Sarajevo na amewahi kupokea tuzo za Knight International Journalism Award, Global Shining Light Award, IRE Award, na European Press Prize. 

Huku hali za dharura zikitangazwa duniani kote na serikali zikipambana kuikabili pandemia ya kirusi cha korona, nafasi mpya za kujifaidi zitajitokeza. Mamia ya mamilioni ya dola zinapangiwa kutumika katika uagizaji wa dharura wa vifaa na matumizi yasiyo wazi ili kukabili kirusi cha korona. Lakini janga hili pia linatoa njia mpya za kuwawajibisha walio mamlakani. Wanahabari wanapaswa kuwa wanaangalia matumizi ya serikali, kuwatambua wazabuni wapya, vyanzo vya huduma au bidhaa zao, na bei zao. Twapaswa kuwa tunaangalia viashiria visivyo vya kawaida – kampuni ambazo hazijawahi kufanya biashara ya vifaa vya matibabu, kampuni zinazomilikiwa kupitia miundo inayohusisha nchi nyinginezo, wazabuni wanaopendelewa kwa kuwa wana uhusiano na watu wenye ushawishi, kampuni ambazo zimekuwa na mauzo ya chini katika miaka ya nyuma, na kadhalika. Kwa kuwa huenda ikawa vigumu kupata habari kutoka kwa serikali, kuongea na washindani na wazabuni walioachwa nje kunaweza kutoa mwelekeo kwa uchunguzi wetu. Lakini kazi yetu haitaisha wakati janga litaisha. Ni hadi mwaka ujao wakati mahesabu yatawasilishwa ambapo tutafahamu kiwango kamili cha jinsi watu walivyojifaidi.

Malachy Browne

Produsa Mwandamizi, Visual Investigations, The New York Times

Malachy Browne.

Browne na timu yake wanaasisi mchanganyiko wa uanahabari wa jadi pamoja na uchunguzi kwa mbinu za kisayansi na kidijitali, kama vile kukusanya na kuchanganua habari kutoka kwa video, picha na nakala za sauti, uchanganuzi wa picha za satelaiti, na kujenga upya maeneo ya matukio ya uhalifu kwa muundo wa 3-D.

Athari za mlipuko wa kirusi cha korona zimefika duniani kote, na pasipokuwapo utangamano wa ana kwa ana, watu wanatangamana kupitia teknolojia na majukwaa ya mitandao ya kijamii. Na kwa hiyo tunaona wazi mvurugo wa maisha ya kila siku, kama inavyodhihirishwa na watu kwa jumla: matukio ya ghasia mipaka inapofungwa, utulivu wa majiji yaliyojaa shughuli na ambayo kwa sasa haina watu, wataalamu wa afya ambao wametuonyesha hali zenye changamoto ndani ya hospitali na hospitali za watu wanaokaribia kufa na vifaa vya kujilinda wanaotengeneza wenyewe, vipindi vya mshikamano wakati wananchi wanawashangilia wafanyakazi kutoka kwenye roshani na nyumbani mwao. Katika siku za mwanzo za mlipuko wa kirusi cha korona, mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ya mtandaoni yaliwawezesha Wachina kuhifadhi na kusambaza habari kuhusu mlipuko ambazo serikali ilikuwa inadhibiti.

Picha za satelaiti na data nyinginezo zinaweza kutuwezesha kupata taswira na kufuatilia athari za kirusi cha korona. Taswira za data ya rununu isiyowatambulisha watu zimeonesha sehemu ambako utunzaji wa umbali wa mtu mmoja hadi kwa mwingine umefanikiwa. Vifuatiliaji vya ndege na data ya abiria pia inaweza kuonesha upungufu wa usafiri wa watu katika umbali mkubwa. Mashirika ya kisayansi yamepima na kutoa taswira ya upungufu wa uchafuzi. Picha za satelaiti na vifaa vya kufuatilia meli vilituwezesha kuonesha ni kwa jinsi gani meli za Korea Kaskazini — ambazo kwa wakati mmoja zilisafiri kwa wingi kuizungukia Uchina — zilikuwa zimerejea na kutia nanga nyumbani, na athari ambazo hilo huenda likasababisha kwa uchumi. Hizi na viashiria vingine na data vina uwezo wa kuonesha kinachofanyika kwa sasa, na kwa kina zaidi kuchanganua ufanisi wa sera mbalimbali za kudhibiti ueneaji wa kirusi cha korona. Na pengine, kwa wakati, kukagua viwango vya mvurugo ambavyo huenda vikavumilika ili kukabili masuala kama vile janga la mabadiliko ya tabianchi. Ni nani ajuaye uvumbuzi utakaotokana na janga hili?

Eliot Higgins

Mkurugenzi Mkuu, Bellingcat

Higgins ameliongoza Bellingcat kuwa mojawapo ya vituo vya upekuzi wa vyanzo vya hadharani vilivyobobea zaidi duniani. Huku likiwa na wapekuzi katika mataifa 20, timu yake imefichua walanguzi wa dawa wakuu nchini Mexico, uhalifu wa kivita nchini Syria, na kudunguliwa kwa ndege ya Urusi MH17.

Jambo moja nimeshuhudia ni jinsi watu wanavyovutiwa na uhakiki wa habari za makala kuhusu kirusi cha korona. Hii ni kwa sababu ya wingi wa madai wanayoyaona yakitolewa na vyanzo mbalimbali, vikiwemo vyombo vya habari, maafisa wa serikali, marafiki na familia zao. Ni vema kutoa mifano ya uhakiki wa kina, lakini pia unaweza kuwasiliana na hadhira moja kwa moja na kuionesha mchakato wenyewe hatua kwa hatua. Msururu wa maandishi kwa Twitter niliyochapisha hivi karibuni nilipokuwa nahakiki picha fulani ulipata umaarufu mkubwa, na ukaniwezesha kuonesha vifaa na mbinu mbalimbali kwa hadhira mpya. Sehemu ya hadhira hiyo iliweza kushiriki na kuhakiki picha tulipokuwa tunaendelea na mchakato wa uhakiki. Huku wengi wetu tukiwa tumelazimika kukaa nyumbani, huu ni wakati mwafaka wa kushiriki katika maonyesho ya moja kwa moja mtandaoni ya upekuzi wetu. Si lazima upekuzi uwe kuhusu madai yaliyo makubwa au muhimu zaidi. Cha msingi ni kuwashirikisha watu katika kila hatua ya safari ya upekuzi wako.

Peter Klein 

Mwasisi na Mkurugenzi Mkuu, Global Reporting Center

Klein aliasisi Global Reporting Centre, shirika lisilo la faida, katika Chuo Kikuu cha British Columbia ili kuvumbua namna uanahabari wa kimataifa unavyoendeshwa. Anaongoza upekuzi kuhusu mifumo ya usambazaji wa vifaa vya matibabu na pandemia, kwa ushirikiano na PBS Frontline na Associated Press.

Uanahabari duniani kote unachukuliwa kuwa “huduma muhimu,” pamoja na wafanyakazi wa afya, maafisa wa serikali, wauzaji chakula, na wengineo wanaohitajika ili kuendesha shughuli za msingi za jamii zetu. Twahitaji kulichukua jukumu hili kwa uzito na kuwajibika ipasavyo. Hii ni nafasi yetu ya kuukabili umati wa watu unaoeneza habari feki na ambao umekuwa ukidhoofisha utendakazi wetu. Uanahabari unaojikita katika uhakiki wa taarifa ni muhimu zaidi kwa sasa kuliko hapo kabla. Kwa hiyo, hakikisha umepata ukweli wa habari husika, na kwa makini utafakari kuhusu ujumbe unaotoa kwa umma.

Mojawapo ya masuala ambayo yamejitokeza wazi katika pandemia ya kirusi cha korona ni ukweli kuwa mifumo yetu ya usambazaji wa bidhaa za matibabu haikuwa tayari kwa janga hili. Mbona hatukuwa tayari, ikizingatiwa watalaamu wa afya ya umma walionya kwa miaka mingi kwamba pandemia ya kimataifa ilikuwa inakuja na ingeuzidi nguvu mfumo wenyewe? Ni nani anayefaidi kwa biashara ya uuzaji wa vifaa vya matibabu na wana jukumu gani katika aidha kusaidia au kuzuia usambazaji wa vifaa vya matibabu vinavyohitajika? Ni nini jukumu la mali miliki katika tasnia inayoendelea kuangazia zaidi mali miliki? Ni hali gani ya mifumo ya usambazaji wa vifaa vya matibabu inayoifanya ishindwe kukabili mabadiliko ya ghafla katika mahitaji?

Wahalifu hutafuta udhaifu katika mifumo, na janga hili kwa hakika limedhihirisha kuwa tu wanyonge. Hitaji la vifaa vya kuokoa maisha linaweza likazidisha ufisadi uliopo serikalini na kwenye mashirika. Ushauri wangu kwa wanahabari duniani kote ni waangalie kazi zao za awali na kutafuta ni nini ambacho huenda kiliwapita. Ikiwa kulikuwa na maafisa fisadi au biashara zilizohusika kwenye kashfa, kwa sasa zina jukumu gani? Janga kama kirusi cha korona linaweza likazidisha utovu wa usawa ambao upo kwa sasa. Mataifa tajiri zaidi na yanayosema kwa sauti ya juu zaidi mara nyingi ndiyo hushughulikiwa – na kupata vifaa. Ni kwa jinsi gani mataifa yenye uwezo mdogo na rasilimali chache yanakabiliana na janga hili, na viongozi wa dunia wanafanya nini kushughulikia utovu wa usawa huu? Hata hivyo, mataifa ambako vifaa vya matibabu hutengenezewa huenda yakawa na ahueni vilevile, na labda kuhodhi vifaa vilivyonuiwa kuuzwa nje ya nchi, ili vitumike ndani ya mataifa hayo wakati wa janga hili. Hali hii itakuwa na athari zake, ambazo yahitaji kuzichunguza.

Jinkyung Byun

Mwanahabari Mpekuzi Mwandamizi, SisaIN (Korea Kusini)

Byun anafanya kazi na SisaIN, jarida la habari la kila wiki linaloongoza nchini humo. Amekuwa kwenye mstari wa mbele akiripoti kuhusu janga la kirusi cha korona nchini mwake. 

Ni vipi na kwa nini kirusi cha korona kinaenea ni maswali muhimu, lakini kirusi cha korona kinaenea kwa kasi mno kiasi cha wanahabari kuweza kuangazia “ni vipi na kwa nini.” Wanahabari wapekuzi wanapaswa kuangazia maswali yanayolenga mbele kuliko kuchanganua kiini chenyewe. Bila shaka, wanahabari wapekuzi sio wabashiri wa mambo yajayo au waaguzi wa maisha ya baadaye ya mtu, lakini twapaswa kutazama mbele na kukadiria nini kitatokea.

Rejeleo bora zaidi la kuegemea wakati tunaangazia mustakabali ni changamoto ambazo nchini nyinginezo zimekubana nazo katika ueneaji wa kirusi. Kwetu sisi, Uchina ndiyo nchi pekee iliyokuwa na ueneaji mkubwa kama Korea Kusini. Lakini mbinu nyingi iliyotumia Uchina – kama vile kufunga majiji, kuminya uhuru wa vyombo vya habari, na kubana haki za kusafiri – hazikuwa chaguzi kwa Korea Kusini kama nchi yenye demokrasia. Ilikuwa pia vigumu kuamini kuwa habari kuhusu kirusi cha korona kutoka Uchina zilikuwa za wazi na huru. Hata hivyo, tungeweza kupata habari kuhusu changamoto zilizoikabili Uchina kutoka kwenye makala za ufanisi zilizochapishwa na vyombo vya habari vinavyodhibitiwa na serikali. Nilidhani kuwa Korea Kusini nayo huenda ilikumbwa na changamoto sawia na kwa hiyo nikaandika makala kuhusu jinsi ya kujiandaa kwa ajili ya shida kama hizo. Kutokana na kuripoti kuhusu pandemia hii, nimegundua kuwa maisha ya watu kutoka nchi moja hadi nyingine hayatofautiani, na matatizo yanayotukabili nayo yanafanana.

Ripoti za upekuzi zinapaswa kujumuisha uchanganuzi linganishi wa mbinu za kila taifa za kukabiliana na kirusi cha korona. Hata hivyo, haitakuwa rahisi kufanya hivi. Hali ya kisiasa, kitamaduni na kiuchumi ambayo kila taifa inaikabili ni tofauti, na kwa hiyo mbinu moja inaweza kuleta matokeo tofauti sana. Wakati wanahabari kutoka nchi fulani huenda wakawa wanajua kuhusu mkutadha kama huo, wanahabari kutoka nchini nyinginezo huenda wasiuelewe na wanaweza fanya uamuzi kwa mujibu wa ripoti ambazo ni za juu juu tu.

Wahabari wapekuzi wana nafasi halisi ya kushirikiana kimataifa. SisaIN, jarida la habari ninalofanyia kazi, ni shirika ndogo na tumekuwa mara nyingi tukiangazia masuala ya hapa nyumbani. Lakini wakati wa pandemia hii, tuliunda kwa haraka mtandao wa waandishi wa ughaibuni – na vilevile waasiliani kutoka makongamano ya uanahabari na uandishi wa habari kutoka ughaibuni – ili watutafutie habari na kutupa michango. Kadhalika, tulichambua majarida ya matibabu ya kimataifa na kuwatumia maswali wataalamu wa afya. Wanapokuwa wakikabili pandemia kama kirusi cha korona, wanahabari wanapaswa kuangalia ni vipi ushirikiano wa kimataifa unahitajika miongoni mwa serikali, wataalamu wa matibabu, na vyombo vya habari: ni aina gani ya ushirikiano inayohitajika, njia mahususi za ushirikiano na vilevile mbinu bora zaidi za utendakazi. Wanahabari wapekuzi walio na mitandao ya kimataifa wanaweza wakafanya jukumu hilo.

Fabiola Torres 

Mwasisi, Salud con Lupa 

Torres ni mkurugenzi na mwasisi wa Salud con Lupa (Health with a Magnifying Glass), jukwaa la kidigitali la uanahabari shirikishi kuhusu afya ya umma lenye makao yake Lima, katika Amerika ya Kilatini. Yeye pia ni mwasisi wa tovuti ya upekuzi yenye umaarufu Ojo Público.

Katika jaribio la kudhibiti pandemia ya kirusi cha korona, nchi nyingi katika Amerika ya Kilatini zimetangaza hali ya dharura. Mbinu hizi zinajumuisha kanuni mpya za matumizi ya fedha za umma (zinazokiuka mchakato wa ukaguzi wa kawaida), kufungwa kwa mipaka, na vizuizi mbalimbali kwa haki za umma na usafiri zinazolenga kuwadhibiti watu wakae waliko kwa lazima. Huu ni wakati mgumu na wenye utata kwa uanahabari wa upekuzi. Naamini kuwa, sasa, kuliko wakati mwingine wowote, twaweza kuuonesha ulimwengu kuwa afya ya umma yapaswa kuchukuliwa kwa uzito. Afya ya umma ni sehemu ya ajenda ya sekta tofauti za jamii na imefungamana sana na uchumi na vilevile siasa za taifa na kimataifa. Afya ya umma yapaswa kuwa mada ya kudumu ya kujadiliwa; ikiwa tutawaza kuhusu afya wakati tu tumeugua au kumekuwa na pandemia, basi tumechelewa sana.

Kwanza, tunapoandika habari za kila siku, lazima tuwe tukijiuliza: Ni jambo gani muhimu zaidi la kuielezea hadhira yangu kwa sasa? Lazima tuzingatie kuwa uanahabari ni huduma ya umma, hasa kwa watu walio wanyonge zaidi na wale walioathirika na dhuluma za kisiasa na kishirika. Pili, lazima tujiulize: Ni nini kilicho hatarini katika pandemia hii? Ni nani anayefaidi kutokana na janga hili la kimataifa? Mashirika ya dawa za matibabu, kampuni za bioteknolojia, na zile zinazotengeneza vifaa vinginevyo vya afya zinapaswa kuchunguzwa kwa makini zaidi kuliko kawaida. Mara nyingi, kanuni zinazoongoza biashara na haki za mali miliki zimekwenda kinyume na maslahi bora ya afya ya umma na haki za binadamu. Wanahabari wapekuzi pia wanahitaji kuangazia matokeo ya athari ya pandemia hii. Kirusi hiki kimeufanya ulimwengu kusimama kabisa. Hali hizi zinasababisha umaskini zaidi na utovu wa usawa kuliko ilivyokuwa awali, na kwa hiyo ni muhimu kuchunguza athari za kiuchumi na za kijamii za pandemia hii.

Pandemia hii imetuonyesha kuwa tunahitaji uanahabari wa upekuzi shirikishi ulio bora, juu ya mada mbalimbali. Katika Salud Con Lupa, tunafanya kazi pamoja na wanahabari kote Amerika ya Kilatini ili kufanya habari ziwe wazi na kutoa zile tu ambazo zimehakikiwa. Vilevile tunashirikiana kwenye miradi ya uanahabari wa upekuzi ili kusaidia katika vita dhidi ya matumizi mabaya ya mamlaka.

Martha Mendoza

Mwandishi wa Kitaifa, The Associated Press 

Mendoza anayefanya kazi kutoka Silicon Valley ni mshindi mara mbili wa tuzo ya Pulitzer, kutokana na makala zake zilizosaidia kuwaweka huru watu 2,000 waliotumikishwa kwenye kiwanda cha vyakula vya baharini cha Thai na kufichua mauaji ya halaiki ya Vita Vya Korea katika No Gun Ri. 

Ushauri wangu wa jumla kwa wanahabari ni ikiwa mwaweza, unganeni. Kuwapo na wenzako mkifanya kazi pamoja wakati huu unaohitaji umakinifu unaipa hadhi kazi yako na unaweza ukaleta ucheshi na ujotojoto katika miingiliano yako ya kila siku.

Kuwapa sauti wasio na sauti hata ni muhimu zaidi. Watu wasio na makazi, wafungwa, na jamii za wahamiaji waliotengwa zinahitaji kufikiwa. Kwa suala la vifaa, nimekuwa nikitumia ImportGeniusPanjivaUSASpendingtrac.syr.eduMarineTraffic, PACER na vinginevyo.

Inapokuja katika uchunguzi wa mifumo ya usambazaji, tumia data na upuuzie mbali madai au semi zilizotiwa chumvi. Wacha simulizi za kusisimua zibaki kuwa simulizi za kusisimua, wala usitoe mahitimisho kutoka kwa chochote isipokuwa takwimu halisi. Tena, hii ni habari ya kimataifa, kwa hiyo ijanibishe, lakini zingatia muktadha mpana. Na kama kawaida rafiki zangu, hebu tutumeni maombi ya kupata habari kupitia Kipengee cha Sheria za Uhuru wa Kupata Habari (FOIAs).

Natalia Antelava

Mhariri Mkuu, Coda Story

Antelava ni mwanahabari wa zamani wa BBC na mwasisi wa Coda Story, shirika vumbuzi lisilo la faida ambalo huchunguza kwa kina mada tofauti sana kama vile vita juu ya sayansi, habari za uongo zitolewazo makusudi, janga la LGBTQ, na uhamiaji.   

Ushauri wangu kwa wanahabari wanaochunguza kirusi cha korona ni kukichukulia kama uchunguzi mwingine wowote. Zifuate fedha na ueleze makala kuhusu watu. Uenezaji makusudi wa habari za uongo ni wa kuzingatiwa kwa sababu unabadilisha jamii zetu. Kama katika janga lolote lile, kuna waathiriwa na wahalifu. Kazi yetu ni kuwatafuta. Ni nini kinachohitaji kuchunguzwa kwa makini zaidi? Ni nini karantini inafanya kwa afya ya akili zetu na jinsi kirusi cha korona kinavyoathiri suala la faragha.

Ying Chan

Profesa Mwenye Enzi, University of Hong Kong

Ying Chan ni mwanahabari, mkufunzi na mwasisi mkurugenzi wa Journalism and Media Studies Centre katika Chuo Kikuu cha Hong Kong. Ameongoza chunguzi za kuenziwa kuhusu spishi zilizo hatarini, ulanguzi wa binadamu, na uhalifu uliopangwa.

Kwa kuanzia, wanahabari wanapaswa kufuata msemo wa zamani wa “fuata fedha.” Jitose kwa kina na uchunguze jukumu la watu walio na maslahi maalum na ya kishirika kwenye masuala ya kufa kupona yanayohusu pandemia ya kirusi cha korona. Kwa mfano, ni nini maslahi ya mashirika katika ukosefu wa vipimo na vifaa vya matibabu? Kuna vipimo vingi sokoni, nchini Marekani na kimataifa. Ni kampuni binafsi gani na watengenezaji wanaotengeneza vipimo hivi? Kuna vikwazo gani katika kutengeneza vipimo kwa wingi? Pia kuna suala la barakoa. Tunahitaji ramani kamilifu zaidi ya mfumo wa usambazaji wa kimataifa, jukumu la maslahi binafsi, madalali, na mashirika. Reuters walikuwa na makala mufti na The New York Times waliripoti kuhusu usambazaji wa vifaa nchini Uchina.

Kuhusu vifaa vya kujikingia, vyombo vya habari vya Marekani viliripoti juu ya usafirishaji kwa mara ya kwanza wa bidhaa kutoka Uchina kwa ndege mwishoni mwa mwezi Machi. Baadaye katika mkutano na wanahabari, afisa mmoja wa Marekani alisema kuwa vifaa hivyo vilikuwa vimepelekwa kwenye soko binafsi, na akakiri kuwa “kumekuwa na tabia isiyo ya kawaida.” Hizo ni tabia kama gani? Wanahabari wamekuwa wakiangazia matukio ya siku kwa siku. Tunahitaji kujizatiti zaidi kupata taswira kamili na tuchunguze kutofaulu kwa wazi kwa mfumo wenyewe.

Susan Comrie

Mwanahabari Mpekuzi, AmaBhungane (Afrika Kusini)

Comrie anafanya kazi na amaBhungane, chumba cha habari cha upekuzi kisicho cha faida nchini Afrika Kusini. Alikuwa kwenye kiini cha mradi wa chumba chake cha habari wa GuptaLeaks, uliofichua kashfa kuu zaidi ya ufisadi kwa miaka mingi, na alitajwa na Sanlam kuwa Mwahabari wa Masuala ya Fedha wa Mwaka barani Afrika.

Uagizaji wa bidhaa wa dharura huunda nafasi nyingi za ufisadi, watu kujifaidi, na matumizi mabaya ya mamlaka. Kwa hiyo nilikuwa nakazia macho kila kandarasi ya dharura au nyongeza za muda wa kandarasi wakati wa kipindi hiki. Nchini Afrika Kusini, Afisi ya Afisa Mwagizaji Mkuu huchapisha nyongeza na michepuko ya kandarasi zote kila robo ya mwaka (zapatikana hapa), lakini huwa inachukua muda mrefu kupata data hii, na kwa hiyo ili kupata matokeo kwa haraka itakubidi kutegemea vidokezi kutoka kwa vyanzo vilivyo ndani.

Jambo lisilotarajiwa na ambalo yapasa kuliangazia ni kanuni za mazingira ambazo zinakiukwa kwa sababu ya kirusi cha korona. Shirika la sheria Webber Wentzel liliandika memo wiki mbili zilizopita na kuonyesha jinsi sehemu za kifungu cha sheria ya Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA) hubadilika wakati wa “hali ya dharura” ambayo tunaambiwa ipo kwa sasa. Kwa hiyo katika suala la wasiwasi kuhusu mazingira, nitaangalia ni nini kinaidhinishwa kwa msingi wa kirusi cha korona, lakini pia nini kingine kinaendelea wakati mamlaka zimezongwa na shughuli za udhibiti wa pandemia.

Syed Nazakat 

Mwasisi na Mhariri Mkuu, DataLEADS (India)

Nazakat huongoza mradi wa uanahabari wa data, DataLEADS, ambao hutoa mafunzo na kuendesha tovuti ya kwanza ya data nchini India inayoangazia uanahabari kuhusu huduma ya afya. Akiwa mwandishi wa The Week, alishinda tuzo ya kifahari nchini India ya Ramnath Goenka Excellence in Journalism Award.

Wanahabari wanakabiliwa na shinikizo kubwa kadiri habari za kila siku zinavyotokea bila kukoma. Lakini cha msingi kwa wanahabari wapekuzi ni kujidhibiti na kumakinika. Usivurugwe na matukio ya kila siku na mikutano ya waandishi wa habari. Chunguza na uchimbue kwa kina zaidi.

Kuna data nyingi inayopatikana kwa sasa. Je, data hii inatueleza nini kuhusu janga linaloendelea? Je, rekodi za umma, stakabadhi, nyaraka za maagizo ya ununuzi ya serikali, na ripoti za mahesabu ya vifaa vya matibabu zinatueleza nini? Je, kuna visa vya utepetevu wa wenye mamlaka na kutotenda? Uanahabari wa upekuzi unaanzia katika kuuliza maswali na kutafuta watu walio na majibu. Inapokuja katika suala la vifaa, nadhani cha msingi ni kuhakiki kila kitu unachopata kupitia vifaa vya kuhakiki vya mtandaoni kama vile InVIDYouTube DataViewerYandexCrowdTangle, sachi za picha kwa kurejea nyuma (reverse image search), na vifaa vya kuhakiki nakala za sauti za lugha ili kutambua matini potovu na maarufu sana mtandaoni. Kila wakati kumbuka kwamba bila kuwa na hakika, hatuna ukweli.

Mojawapo wa taarifa ambazo wanahabari wanapaswa kuangazia zaidi ni biashara ya wanyamapori ya kimataifa, ikizingatiwa kirusi cha korona kilisababishwa nao, na magonjwa mengine mengi ya maambukizi baina ya binadamu na wanyama yalisababishwa na wanyamapori. Katika kipindi cha miaka iliyopita, kiwango cha biashara ya wanyamapori hai, hata iliyo halali, kimeongezeka na hatuna taswira kamili ya ukubwa wake na athari zake kwa afya ya binadamu.

Musikilu Mojeed 

Mhariri Mkuu, Premium Times – Nigeria

Mojeed ni mmoja wa wanahabari wapekuzi wanaoongoza nchini Nigeria na ameripoti kuhusu ufisadi, haki za binadamu na ulanguzi wa binadamu. Miongoni mwa sifa zake ni kupewa tuzo za Global Shining Light Award, Wole Soyinka Investigative Reporting Award, na Data Journalism Award. 

Naamini huu ni wakati kwa wanahabari kufuata mabilioni ya fedha zinazotolewa nchini mwao ili kukabiliana na pandemia ya kirusi cha korona. Nchini Nigeria, kwa mfano, muungano wa sekta binafsi ulitoa msaada wa Naira za Nigeria bilioni 15 (takriban dola milioni 39 za Marekani) kwa serikali kuu ili kusaidia juhudi zake za kujenga vituo vya kutengea watu vilivyo na vifaa vya kutosha, na kuagiza vifaa na dawa zinazohitajika kupiga vita ugonjwa huu. Fedha nyingi zinakusanywa na kutumika na kuna uwezekano wa baadhi ya maafisa kupanga njama ya kujitajirisha kinyume cha sheria.

Naamini hali zinafanana katika nchi zetu nyingi. Wanahabari lazima waendeleee kufuatilia matumizi na taratibu za uagizaji za maafisa wakuu. Mara nyingi, maafisa wakuu huwa na mazoea ya kufuja au kuiba waziwazi fedha za umma katika nyakati za dharura kama hii. Mataifa mengine pia yanatoa kwa wingi fedha za kutafitia na kufanyia vipimo vya matibabu. Ingefaa kufuatilia matumizi haya kwa lengo la kubaini jinsi dunia inavyofaidi na matumizi hayo. Wanahabari lazima wahakikishe kuwa pandemia yenyewe haikuishia kuwatajirisha maprofesa wazembe waliopokea fedha za kutafitia lakini hawakufanya lolote.

Wanahabari pia lazima wawe makini na kuangazia ukiukwaji wa haki za binadamu unaoendelea wakati huu duniani kote. Nchi nyingi zimeweka amri za kutotoka nje na kuwahusisha polisi, wanajeshi na idara nyinginezo za usalama ili kutekeleza sera zinazowataka watu kusalia nyumbani. Kuna ripoti kuwa idara za usalama katika baadhi ya mataifa zinazidi kutumia nguvu kupita kiasi na kudhulumu haki za wananchi. Wanahabari wana wajibu wa kunakili dhuluma hizi.

Rawan Damen 

Mkurugenzi Mkuu, Arab Reporters for Investigative Journalism

Damen anayefanya kazi kutoka Amman huongoza ARIJ, kituo cha uanahabari wa upekuzi kisicho cha faida kinachoongoza katika Mashariki ya Kati. Kwa miongo miwili amefanya kazi kama mtengenezaji filamu, huku akitayarisha na kuelekeza zaidi ya saa 30 za makala za video za Al Jazeera Media Network na wengineo.

Hii ndiyo habari kuu zaidi mwaka wa 2020 na pengine huenda itabakia hivyo kwa miaka mingi ijayo. Hii sio habari ya afya au ya kisayansi; hii ni habari ya kijamii, kisiasa na kiuchumi; ni habari ya haki za binadamu, jamii na utamaduni. Ushauri wangu wa kwanza ni kuhakikisha kwamba wewe upo ili kuandika taarifa wala usiwe “taarifa yenyewe” kwa kuhatarisha afya yako. Kuna hitaji kubwa la ufafanuzi wa habari, kwa kuwa taarifa kuhusu kirusi cha korona zinasomwa/kutazamwa na zitasomwa/kutazamwa kwa wingi. Vilevile kuna nafasi bora ya ushirikiano ukiukao mipaka ya mataifa kwa kuwa wanahabari wanaandika kuhusu habari moja, na wengi wao hawawezi wakasafiri nje ya nchi zao. Wakati uo huo, ni muhimu kujiuliza ni nini kinafanya taarifa yako kuwa ya pekee. Kadhalika, hii ni hali inayobadilika kwa kasi na kwa hiyo tunahitaji kufanya upekuzi ndani ya muda mfupi hata ingawa tunahitaji kufanya upekuzi wa muda mrefu ambao uhai wake utadumu kwa muda mrefu.

Kwa wale wanaofanya upekuzi wakiwa nyumbani, bila uwezo wa kwenda kwenye matukio, usituambie wanachojua wataalamu, tueleze ni vipi wanavyojua. Usiangazie muundo tu bali kilichopelekea muundo wenyewe; sio tu takwimu, lakini muktadha wake. Changanua kwa makini wanachosema maafisa wa afya na wanasiasa na uwawajibishe. Ni muhimu kujirakibisha na matumizi ya simu na vifaa vya kidijitali kama Signal, Jitsi na Zoom kuwasiliana na vyanzo vyako. Huu ni wakati wa kuunda uhusiano na vyanzo vipya na kadiri unavyoweza. Hatimaye, jihadhari usiwanyanyapae walioambukizwa au usifanye ubaguzi wa rangi katika taarifa zako.

Makala hii imetafsiriwa na Kabugi Mbae, mwanahabari wa Kenya na mwanachama wa Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU).

 

Republish our articles for free, online or in print, under a Creative Commons license.

Republish this article


Material from GIJN’s website is generally available for republication under a Creative Commons Attribution-NonCommercial 4.0 International license. Images usually are published under a different license, so we advise you to use alternatives or contact us regarding permission. Here are our full terms for republication. You must credit the author, link to the original story, and name GIJN as the first publisher. For any queries or to send us a courtesy republication note, write to hello@gijn.org.